Uhamiaji Marekani: Trump akumbana na pingamizi za kisheria
7 Septemba 2025Rais wa Marekani Donald Trump ameahidi kufukuza mamilioni ya wahamiaji kwa mpango mkubwa zaidi wa kuondoa watu kihistoria. Lakini ajenda yake ya uhamiaji inakabiliwa na majaribu makubwa mahakamani, huku sera nyingi zikizua kesi na maamuzi ya mahakama.
Wiki iliyopita, Mahakama ya Rufaa ya Marekani iliamua kuwa utawala wa Trump hauwezi kutumia sheria ya vita ya karne ya 18 kuharakisha kufukuza raia wa Venezuela wanaodaiwa kuwa wanachama wa genge la Tren de Aragua. Uamuzi huo sasa unasubiri mapambano mapya katika Mahakama ya Juu.
Baadhi ya sera za rais zinawaathiri mamia ya maelfu, au hata mamilioni ya watu. Wanasheria wa haki za wahamiaji wamesema hatua za Trump zinapuuza katiba na haki za binadamu, huku Ikulu ikisisitiza kwamba rais ana mamlaka ya kulinda usalama wa taifa.
Mfano wa hivi karibuni ni kesi ya Alien Enemies Act ya mwaka 1798, ambayo utawala wa Trump ulitumia kuondoa raia waliotajwa kama washiriki wa magenge, ikiwapeleka moja kwa moja gerezani Amerika ya Kati. Mahakama imekataa tafsiri hiyo, ikisema sheria hiyo haikukusudiwa kutumika dhidi ya magenge.
Lee Gelernt wa ACLU alisema uamuzi huo umedhibiti mtazamo wa utawala kwamba unaweza kutangaza dharura bila uangalizi wa mahakama. Hata hivyo, msemaji wa White House Abigail Jackson alisisitiza rais ana mamlaka ya kuondoa magaidi na kulinda taifa.
Hatua tata ya uraia wa kuzaliwa
Trump pia alitoa amri ya kiutendaji kujaribu kufafanua upya uraia wa kuzaliwa chini ya marekebisho ya 14 ya katiba ya Marekani. Utawala wake ulidai kwamba watoto waliozaliwa Marekani si raia iwapo wazazi wao hawana hadhi ya kisheria.
Mataifa kadhaa yakiwemo Washington, Arizona, Illinois na Oregon yalishtaki, yakisema agizo hilo linapuuza maandiko ya katiba na uamuzi muhimu wa Mahakama ya Juu wa mwaka 1898 uliothibitisha uraia wa mtoto aliyezaliwa San Francisco kwa wazazi Waki-China.
Mwishoni mwa Julai, mahakama ya rufaa mjini San Francisco ilitupilia mbali amri ya Trump, ikisema ni kinyume cha katiba. Uamuzi huo uliidhinisha hukumu ya awali kutoka New Hampshire iliyozuia utekelezaji wa agizo hilo nchini kote.
Hii ilikuwa pigo kubwa kwa sera ya Trump, huku wapinzani wakisema hatua hiyo ingeunda "uraia wa daraja la pili” na kuzua mamilioni ya watu wasio na taifa.
Utawala wa Trump umeapa kupeleka kesi hii hadi Mahakama ya Juu, ukisema agizo lake linakusudia "kulinda uadilifu wa taifa na katiba.”
Kufukuzwa kwa nchi ya tatu
Sera nyingine yenye utata ni ile ya kuwasafirisha wahamiaji hadi nchi ambazo hawana uhusiano nazo, ikiwemo El Salvador na Sudan Kusini. Maafisa wa serikali walisema hatua hii inalenga wahamiaji wanaotoka nchi zisizokubali kuwapokea tena au waliokutwa na makosa ya jinai.
Mashirika ya haki za wahamiaji yalisema sera hii inakiuka haki ya mchakato wa kisheria, na kwamba inahatarisha maisha ya wahamiaji kwa kuwapeleka katika mataifa yenye historia ya ukiukaji wa haki.
Machi mwaka huu, jaji wa shirikisho alizuia kwa muda kufukuzwa kwa wahamiaji hadi nchi ya tatu bila wao kusikilizwa, lakini Mahakama ya Juu ilisitisha agizo hilo Juni, ikiruhusu kufukuzwa kwa haraka.
Wanasheria wa wanaume watano waliotupwa Eswatini walisema wameshikiliwa kwa wiki saba bila mashtaka wala msaada wa kisheria. Moja ya mataifa yao ya asili, Jamaica, lilikuwa tayari kuwapokea tena, lakini walikuwa tayari wamehamishwa.
Wakosoaji wamesema hatua hii inahatarisha maisha na inaleta picha ya Marekani kupuuza wajibu wake wa kimataifa.
Uvamizi wa California
Mapema mwaka huu, mamlaka ya uhamiaji Marekani ilifanya msako mkubwa Kusini mwa California, ikiwakamata wahamiaji wengi hasa wa asili ya Kilatino kutoka maeneo kama vituo vya magari, Home Depot na vituo vya mabasi. Mashirika ya haki yalisema hata raia wa Marekani walikumbwa kwenye misako hiyo.
Mashirika ya kutetea wahamiaji yalishtaki, yakiilamu serikali kwa kulenga watu kwa misingi ya rangi na asili ya kikabila. Wizara ya Sheria ilitetea hatua hiyo, ikisema maafisa wana ruhusa kuzingatia vigezo kama kazi au eneo lenye kipaumbele cha kiusalama.
Jaji wa shirikisho aliamuru kusitishwa mara moja kwa mbinu hizo katika kaunti saba ikiwemo Los Angeles, akisema zinakiuka katiba ya Marekani. Mahakama ya rufaa ilithibitisha uamuzi huo.
Hata hivyo, utawala wa Trump uliomba Mahakama ya Juu kusitisha amri hiyo, ukidai imewafunga mikono maafisa wa uhamiaji katika kushughulikia uhalifu.
Suala hili sasa linasubiri maamuzi ya mwisho ya Mahakama ya Juu, likiwa na athari kubwa kwa haki za wahamiaji kote nchini.
TPS na kufukuzwa kwa haraka
Trump pia ameshinikiza kumaliza hadhi ya ulinzi wa muda inayojulikana kama Temporary Protected Status (TPS) kwa zaidi ya watu milioni 1.5. Hii ni hadhi inayoruhusu wahamiaji waliopo Marekani kubaki na kufanya kazi iwapo nchi zao zinakumbwa na vita au majanga.
Mei mwaka huu, Mahakama ya Juu iliruhusu utawala kuondoa TPS na ruhusa za kibinadamu wakati kesi zikiendelea, jambo lililozua hofu kubwa miongoni mwa wahamiaji.
Lakini mwishoni mwa wiki, jaji wa shirikisho Edward Chen alirejesha ulinzi wa TPS kwa Wavenezuela na Wahaiti milioni 1.1, akisema waziri wa usalama wa ndani hakuwa na mamlaka ya kisheria kufuta uamuzi wa awali. Mahakama ya Rufaa ya tisa pia iliunga mkono uamuzi huo.
Sambamba na hilo, wizara ya usalama wa ndani ilipanua matumizi ya sera ya expedited removal – kufukuzwa kwa haraka bila wahamiaji kusikilizwa na jaji. Hatua hii pia imezua kesi nyingi, huku majaji wa shirikisho wakisema inakiuka haki za msingi za mchakato wa kisheria.
Jaji Jia Cobb alisema swali la msingi ni iwapo wahamiaji waliokimbia dhuluma wanapaswa kupewa nafasi ya kusikilizwa ndani ya mfumo wa kisheria.
Vita vya kisheria vinaendelea
Kwa jumla, sera za uhamiaji za Rais Trump zimezua wimbi la migogoro ya kisheria kote Marekani. Kuanzia uraia wa kuzaliwa, hadi kufukuzwa kwa haraka na kuondolewa kwa TPS, kila sera inazusha mashauri mapya mahakamani.
Wakosoaji wanasema hatua hizi zinatishia misingi ya katiba na kuunda mamilioni ya watu wasio na taifa. Utawala wa Trump unasema sera hizo ni za muhimu kwa usalama wa taifa na kulinda maslahi ya Marekani.
Hatua ya Mahakama ya Juu sasa inabaki kuwa kipimo cha mwisho cha kuamua iwapo mipango ya Trump itaendelea au itazuiwa kabisa. Kwa sasa, wahamiaji mamilioni na familia zao wanabaki katika hali ya wasiwasi, wakisubiri uamuzi wa mwisho wa mahakama kuu.
Chanzo: APE