Senegal yasaini makubaliano mapya na waasi wa Cassamance
28 Februari 2025Dakar imeyataja makubaliano hayo kuwa hatua muhimu ya kuelekea kumaliza mmoja wa migogoro ya miaka mingi barani Afrika. Hata hivyo, wachambuzi wanasema makubaliano hayo hayakuyashirikisha makundi yote ya waasi na yameshindwa kushughulikia chanzo cha matatizo yaliyosababisha mgogoro huo.
Serikali ya Senegal kupitia Waziri Mkuu, Osmane Sonko imesaini makubaliano hayo na kundi la waasi wa vuguvugu la wanaopigania demokrasia katika mkoa wa Cassamance, wakati alipokwenda ziarani nchi jirani ya Guinea Bissau wiki hii.
Makubaliano yaliyowahi kufikiwa huko nyuma kati ya pande hizo mbili yalishindwa kumaliza vita katika mkoa huo ambao uko baina ya Senegal na Gambia.
Waasi wa Cassamance wamekuwa wakipambania uhuru wao tangu mwanzoni mwa miaka ya 1980 kutokana na kupuuzwa kimaendelea na serikali mjini Dakar.