Scholz na Zelensky wakubaliana umuhimu wa Trump kwenye amani
5 Machi 2025Taarifa iliyotolewa na msemaji wa serikali ya Ujerumani imeeleza kuwa Scholz, anayemaliza muda wake ameyathibitisha hayo Jumatano katika mazungumzo yake ya simu na Zelensky na kusema Trump ni mtu muhimu katika mazungumzo ya amani na Urusi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Scholz amepongeza hatua ya Zelensky kuonyesha nia ya kufanya mazungumzo mapema iwezekanavyo.
Viongozi hao wote wawili wamekubaliana umuhimu wa nafasi ya uongozi wa rais wa Marekani, pia kwa nia ya kufikia haraka makubaliano ya kusitisha mapigano na kupatikana amani ya kudumu Ukraine. Scholz alisisitiza pia kuendeleza mshikamano usioyumba wa Ujerumani na Ukraine.
Ufaransa, Uingereza, Ukraine na juhudi za kuumaliza mzozo
Ama kwa upande mwingine, ofisi ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron imesema kuwa kiongozi huyo hana mpango wa haraka wa kwenda Marekani pamoja na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer, katika juhudi za kidiplomasia za kuharakisha mchakato wa kuvimaliza vita vya Urusi dhidi ya Ukraine.
Mapema Jumatano, msemaji wa serikali ya Ufaransa, Sophie Primas, aliwaambia waandishi habari baada ya mkutano wa baraza la mawaziri kwamba kulikuwa na uwezekano Macron akarejea Washington akiongozana na viongozi wenzake wa Ukraine na Uingereza, ingawa safari hiyo bado haijapangwa.
Macron alikutana na Trump mwezi Februari katika Ikulu ya Marekani, White House, katika juhudi za kuharakisha masharti ya awali ya makubaliano ya amani na Ukraine.
Muda mfupi baada ya ziara yake, Starmer naye aliizuru Marekani, ambako alisema mkutano baina yake na Trump ilikuwa wenye manufaa. Viongozi hao wawili wa Ulaya walikuwa katika juhudi za kufungua njia kwa mkutano wa Zelensky na Trump, ambao hata hivyo, ulimalizika vibaya kwa majibizano.
Urusi yapongeza utayari wa Zelensky
Wakati huo huo, Ikulu ya Urusi, Kremlin imepongeza taarifa kwamba Rais Zelensky yuko tayari kusaini mkataba wa madini na usalama. Mapema Jumatano asubuhi, msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov, alisema Urusi inaichukulia hatua hiyo kama iliyo njema.
''Barua ya Zelensky ilikuwa nzuri. Swali ni nani wa kuzungumza naye. Hadi kufikia sasa, rais wa Ukraine bado amepigwa marufuku kisheria kuzungumza na upande wa Urusi. Kwa hivyo, mtazamo wa jumla ni mzuri, lakini ajenda bado haijabadilika,'' alifafanua Peskov.
Rais wa zamani wa Urusi, Dmitry Medvedev amesema lengo la nchi yake linabakia kuwa lile lile la kuishinda Ukraine. Medvedev ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Usalama lenye nguvu la Urusi, amesema nchi hiyo inazidi kusonga mbele.
Matamshi hayo ameyatoa baada ya Wizara ya Ulinzi ya Urusi kudai kuwa wamesonga mbele kidogo katika jimbo la Donetsk lililoko Ukraine. Medvedev amesema pia anatarajia Marekani itarejesha msaada wake kwa Ukraine, ikiwa Kiev na Washington zitasaini mkataba wa madini.
Katika hatua nyingine viongozi wa Ulaya wanatarajia kukutana kesho katika mkutano wao wa kilele utakaojadili masuala ya ulinzi na mzozo wa Ukraine.
(AFP, DPA, AP, Reuters)