Scholz na Merz wachuana kwenye mdahalo wa Televisheni
10 Februari 2025Kansela Olaf Scholz amemshutumu mpinzani wake mkubwa wa kisiasa Fredrich Merz kwa kuvunja ahadi yake kwa kukubali uungaji mkono kutoka chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD, kusukuma muswaada wake wa kufanya mabadiliko katika sera ya uhamiaji, bungeni.
Katika mdahalo wa kwanza wa televisheni kati ya wanasiasa hao,Merz aliweka wazi mipango yake ya kuleta mabadiliko nchini Ujerumani.
Wagombea wawili wakuu wa Ukansela,nchini Ujerumani Olaf Scholz na mpinzani wake Fredrich Merz, walichuana kwenye mdahalo wa kwanza wa televisheni usiku wa kuamkia leo uliojikita kuanzia siasa za ndani, uhamiaji,Uchumi, sera za kigeni na mahusiano na Marekani.
Katika mjadala kuhusu sera ya uhamiaji Kansela Olaf Scholz wa chama cha Social Democratic, SPD alimlaumu mpinzani wake akiwaomba wapiga kura wafikirie mara mbili kuhusu mgombea huyo wa CDU, akisisitiza kwamba hawezi kuaminika kutokana na hatua yake ya hivi karibuni ya kuruhusu kuungwa mkono na chama cha AfD katika muswaada aliyouwasilisha bungeni wa mageuzi ya sera ya uhamiaji.
"Na kwa kuizingatia historia yetu, sisi kama wajerumani tunapaswa kufanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba AfD haina nguvu. Hiyo ndiyo sababu hakuna ushirikiano na chama hicho. Mnaweza kukitumainia chama cha Social Democratic na mnaweza kunitumainia mimi.
Mpinzani wake kutoka chama cha kihafidhina cha Christian Democratic Union CDU, Fredrich Merz kwa mara nyingine kwenye mjadala huo,nae akasisitiza kwamba hawezi kuunda serikali na Afd ikiwa wapiga kura watampa idhini ya kuwa Kansela,lakini akasisitiza kwamba vyama vingine vikubwa vitakavyoingia bungeni vitalazimika kujitolea ili kuizuia Afd.
''Tatizo hapa na tumelitaja tangu mwanzo, ni AfD. Wakati bwana Scholz alipoanza,AfD walikuwa kwenye asilimia 10.3. Hivi sasa bwana Scholz anaondoka, AfD inashikilia asilimia 20. Hiki ni kitisho kikubwa kwa demokrasia yetu.AfD lazima idhoofishwe tena.''
Wagombea wote wawili kwa kiasi kikubwa walionekana kuwa kwenye ukurasa mmoja katika masuala mengi yanayohusu sera za kigeni.
Kuhusu vita vya Ukraine Kansela Olaf Scholz alisema Ujerumani ni muungaji mkono mkubwa wa nchi hiyo barani Ulaya na itaendelea kuwa hivyo.Soma pia:Changamoto za kisiasa zinazoisubiri Ujerumani mwaka 2025
Alifafanuwa kwamba bado vita hivyo ni hatari na Ujerumani na Ulaya wanapaswa kupambana kila siku kuzuia visitanuke kuwa vita kati ya Urusi na jumuiya ya NATO.
Fredrich Merz upande wake aliweka mkazo kwamba Urusi ni kitisho kikubwa kwa usalama kwa mataifa ya Ulaya na kubaini kwamba wanapaswa kujiandaa kwa miaka kadhaa ijayo dhidi ya Urusi.
Kwenye uchumi kila mmoja amejitapa kuwa mtu sahihi atakayeimarisha hali ya uchumi inayoyumba. Japo Fredrich Merz alimkosoa Scholz kwamba sera zake zimechangia pa kubwa katika kuuporomosha uchumi wa Ujerumani.
Wagombea wote wawili wakitowa mitazamo yao kuhusu mahusiano na rais wa Marekani Donald Trump, walionesha kuwa tayari kushirikiana na rais huyo japo pia walisisitiza juu ya umuhimu wa kuifanya Ulaya kuwa imara na isiyoyumbishwa na Marekani.
Kansela Olaf Scholz alilitaja pendekezo la Trump la kutaka kuchukuwa umiliki wa Gaza na kuwahamisha Wapalestina, kama pendekezo la fedheha huku mpinzani wake Fredrich Merz akizungumzia kutoridhishwa kwake na pendekezo hilo akiiliita ni la kimabavu lakini pia akaongeza kusema kwamba tunabidi kusubiri na kuona kitu gani kitatokea na vipi mpango huo utatekelezwa.
Scholz na Merz ni wagombea wawili wakuu watakaopambana katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani Februari 23.