Scholz na Merz wachuana katika mdahalo kuelekea uchaguzi
10 Februari 2025Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kutoka chama cha SPD na mpinzani wake mkuu Friedrich Merz kutoka kambi ya kihafidhina ya vyama vya CSU/CDU wamekabiliana jana katika mdahalo wa moja kwa moja kwa njia ya televisheni kabla ya uchaguzi wa Februari 23.
Scholz amemshutumu Merz kwa kuvunja kauli yake baada ya kukubali kuungwa mkono na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD, wakati akishinikiza pendekezo la kupinga uhamiaji kupitia bunge.
Kwa upande wake Merz, amesisitiza kuwa chama chake cha Christian Democratic Union CDU na washirika wao wa Bavaria CSU, iwapo watashinda uchaguzi hawatashirikiana au kutawala na AfD inayopinga wahamiaji.
Wagombea hao wawili walichuana kuhusu masuala ya uchumi, sera za kigeni, matumizi ya ulinzi, na jinsi Berlin inapaswa kukabiliana na Rais wa Marekani Donald Trump.