Scholz Katika mapambano ya Ukansela wa Ujerumani
20 Februari 2025Septemba 2024, Olaf Scholz wa SPD aliulizwa swali kuhusu kile alichotarajia siku moja kingeandikwa kwenye vitabu vya historia kuhusu ukansela wake.
Jibu fupi na kavu la kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 66 sasa lilikuwa: "Nadhani mtu anapaswa kuwa mwangalifu na wanasiasa wanaofikiria juu ya hilo kabla au wakati wa muda wao madarakani.
Hivi sasa, muungano wake wa SPD, Kijani, na FDP umevunjika, na uchaguzi wa mapema utafanyika Februari 2025. SPD iko nyuma kwenye uchunguzi wa maoni ya wapigakura dhidi ya CDU/CSU na katika baadhi ya maeneo, chama cha AfD.
Soma pia:Merz akemea kauli za Musk kuunga mkono AfD katika uchaguzi Ujerumani
Scholz ana imani ya kushinda, akikumbuka ushindi wake wa 2021 ambapo kura za maoni zilionesha SPD ilikuwa inaungwa mkono kwa asilimia 15, lakini kilishinda.
Scholz anaendelea kuwakumbusha wapiga kura hilo katika kampeni ya 2025. Lakini wakati huu, hakuonekani kutokea maajabu.
Ili kuinua uchumi dhaifu, SPD inataka kupunguza vikwazo vya ukopaji na kupata mapato kupitia mikopo ya serikali, kama Scholz alivyoelezea. Katika sera za kigeni, Scholz anaahidi busara, hasa kuhusu utoaji wa silaha kwa Ukraine bila kusababisha mgogoro wa moja kwa moja.
Mzozo wa nishati Ujerumani chini ya Scholz
Scholz alikuwa amekalia kiti cha Kanzala kwa miezi mitatu tu wakati Ukraine ilipovamiwa na Urusi Februari 2022, na tangu wakati huo nchi inakabiliana na mzozo wa nishati, mfumuko wa bei, na matatizo mengine.
Muungano wa trafiki wa vyama vya SPD, Kijani, na FDP - ulikuwa na migogoro ya mara kwa mara, na hatimaye ukawa serikali isiyopendwa zaidi nchini.
Ingawa umakini wa wananchi ulikuwa mkubwa, Scholz hakujali sana matokeo ya tafiti za umma, akisema kila kitu kinawezekana. Safari yake ya kisiasa ilianzia tawi la vijana la chama cha SPD, linalojulikana kama JUSO, kabla ya kuanza kazi kama wakili wa sheria ya kazi na kujifunza kuhusu uchumi na ujasiriamali.
Soma pia:Chama cha Kijani Ujerumani chakamilisha ilani ya uchaguzi
Alifanya kazi kama Seneta wa Ndani wa jimbo la Hamburg, Waziri wa Kazi, na baadaye kuwa Meya wa Hamburg kabla ya kurudi Berlin kama Waziri wa Fedha na Naibu Kanzala. Wakati akiwa Katibu Mkuu wa SPD, alitambuliwa kama "Scholzomat" kutokana na mtindo wake wa kitaaluma na baridi.
Viwango vya chini vya umaarufu wake vilisababisha baadhi katika chama cha SPD kujiuliza iwapo chama hicho kinaweza kuwa bora zaidi kuelekea uchaguzi wa shirikisho wa 2025 kikiongozwa na Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius.
Pistorius amekuwa mwanasiasa maarufu zaidi nchini Ujerumani katika kura za maoni kwa miezi kadhaa. Lakini Scholz hakuruhusu kuachia nafasi yake ya kugombea.