Saudi Arabia yawanyonga wanane kwa ulanguzi wa mihadarati
3 Agosti 2025Saudi Arabia imewaua kwa kuwanyonga watu wanane ndani ya siku moja, ikiwa ni sehemu ya ongezeko la matumizi ya adhabu ya kifo nchini humo hasa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya.
Shirika la habari la Saudi SPA limeripoti kuwa raia wanne wa Somalia na Waethiopia watatu walinyongwa jana Jumamosi katika eneo la Najran, kusini magharibi mwa nchi hiyo kwa kosa la "kuingiza bangi nchini humo kwa njia za magendo."
Aidha mwanamume mmoja raia wa Saudi alihukumiwa kunyongwa kwa kosa la kumuua mama yake.
Kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la AFP, tangu mwanzoni mwa mwaka huu 2025, Saudi Arabia imewahukumu watu 230 kunyongwa. Idadi kubwa ya watu walionyongwa – 154 – walihusishwa na makosa yanayohusiana na ulanguzi wa dawa za kulevya.
Kasi ya utekelezaji wa adhabu ya kifo kwa kunyongwa inaonyesha utawala huo wa kifalme uko katika mwelekeo wa kuvunja rekodi ya mwaka jana ambapo watu 338 walinyongwa.
Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (OHCHR) imelaani vikali kurejeshwa kwa adhabu ya kifo kwa makosa ya ulanguzi wa dawa za kulevya, ikisema ni kinyume na sheria ya kimataifa.