Sare ya mashule haziwezi kuchukua nafasi ya siasa nzuri ya kijamii"
8 Mei 2006Kuhusu namna Rais Goerge W. Bush wa Marekani alivyozungumza katika vyombo vya habari vya Ujerumani, gazeti la Braunschweiger Zeitung limeandika:
“Inaonekana George Bush hataki kuanzisha mabishano tena. Kwa hivyo, anafuata mapendekezo ya washauri wake ya kuisifu Ujerumani karibu kupita kiasi. Ghafla Ujerumani ina umuhimu katika kuupiga vita ugaidi duniani. Na vile vile Bush anausifu msimamo mkali wa Ujerumani dhidi ya Iran. Ni rahisi sana kufahamu mkakati wa Bush: Anajaribu kuwashawishi Wajerumani kuwa marafiki. Lakini mahusiano kati ya Ujerumani na Marekani ni mazuri na yatabaki kuwa hivyo, siyo kwa sababu ya rais Bush, lakini licha yake!”
Na gazeti la “Der neue Tag” la mjini Weiden limeandika, licha ya maneno ya maridhiano, bado Rais Bush atashindwa kupata sura nzuri nchini Ujerumani. Mhariri huyu anasema:
“Rais wa Marekani amejitambulisha kama mtu anayefahamu hisia za Wajerumani akizungumzia msimamo wa Wajerumani dhidi ya vita vyote, na serikali ya Ujerumani kukataa kushiriki katika vita dhidi ya Irak. Maneno yake yanaonyesha kuwa amefanya uchunguzi barabara wa maoni ya jamii ya Kijerumani. Bila shaka, ameelewa pia kuwa ni vigumu sana kwa rais yoyote wa Marekani kuaminiwa na Wajerumani, ikiwa ni Bush au mrithi wake, kwani Wajerumani wana wasi wasi juu ya namna Wamarekani wanavyoitawala dunia.”
Na juu ya pendekezo la waziri wa sheria kwamba wanafunzi wa hapa nchini wavae yunifomu au sare mashuleni kuna maoni tofauti. Gazeti la “Kölnische Rundschau”, kwa mfano, linakubali pendekezo hilo likiandika:
“Kutokana na historia yake Wajerumani wana wasi wasi kuhusu kuvaa yunifomu. Lakini mbona tusijaribu, na tuwahusishe wanafunzi pia, kwani inasemekana nguo sawa sawa zinasaidia kujenga umoja kati ya wanafunzi.”
Mhariri wa gazeti la “Westdeutsche Zeitung” la mjini Düsseldorf lakini ana maoni mengine. Ameandika:
“Huwezi kukataa hoja zinazotoa sababu za uzuri wa yunifomu. Lakini kwa upande mwingine: vipi sare zinasaidia? Yule anayeamini yunifomu inaweza kusaidia tofauti za kijamii zisahauliwe, tayari anakubali kushindwa kupigania usawa wa kijamii. Yunifomu haziwezi kuchukua nafasi ya siasa nzuri ya kijamii.”