Sane asafiri na Bayern licha ya atiati kuhusu mkataba wake
10 Juni 2025Sane alijumuishwa katika orodha ya wachezaji 29 wa Bayern watakaosafiri kuelekea Orlando, ambako watakita kambi yao kwa ajili ya mashindano hayo.
Mkataba wa Sane unakamilika Juni 30 huku mashindano hayo ya Kombe la Dunia la Vilabu yakiwa wanaanza Juni 14 na kufikia mwisho Julai 13.
Kulingana na ripoti, Sane mwenye umri wa miaka 29 hivi majuzi aliukataa mkataba aliopewa na Bayern ambao ungemuweka hapo Allianz Arena hadi mwaka 2028.
Bayern ilikuwa inamshinikiza Sane aweke kila kitu peupe kabla safari hiyo ya Marekani, ila bado haijawa wazi iwapo Mjerumani huyo ataendelea kuwa mchezaji wa Bayern msimu ujao au la.
Sehemu ya kwanza ya kikosi ikiwajumuisha Jamal Musiala, Manuel Neuer na Thomas Müller wanasafiri leo ila wachezaji ambao bado wapo na timu zao za taifa kama vile mshambuliaji Harry Kane, watajiunga na kikosi katika siku chache zijazo.
Bayern watakuwa wanapambana na Auckland City katika mechi yao ya kwnaza ya makundi mnamo Jumapili.