SAMARRA: Msako wa waasi unaendelea nchini Iraq
4 Juni 2005
Wairaqi 19 wameuawa katika machafuko yaliozuka sehemu mbali mbali nchini Iraq tangu siku ya Alkhamis.Mtoto mmoja ni miongoni mwa Wairaqi waliouawa,katika opresheni ya vikosi vya Marekani na Iraq ya kuwasaka waasi.Duru za kijeshi za Marekani zimesema,mtoto huyo aliuawa katika mapambano yaliozuka kati ya waasi na polisi katika mji wa Samarra.Kwa mujibu wa maafisa wa Kiiraqi,katika msako uliofanywa na vikosi vya serikali wiki iliyopita katika mji mkuu Baghdad,watu wapatao 700 wamekamatwa na wengine 28 wameuawa.Ripoti zingine zasema kuwa kusini mwa Baghdad,wanajeshi 800 wa Kiiraqi na Marekani wameanzisha mashambulio dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuwa ni wanamgambo.Kwa wakati huo huo,gazeti la Marekani,“Washington Post“ limemnukulu waziri wa ndani wa Iraq akisema kuwa Wairaqi 12,000 wameuawa katika mashambulio mbali mbali ya waasi katika kipindi cha miezi 18 ya nyuma.