SADC yaweka mikakati ya kuimarisha amani
25 Julai 2025Mkutano wa 27 wa Kamati ya Mawaziri wa Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umehitimishwa rasmi jijini Dar es Salaam, ambapo mawaziri kutoka nchi 16 wanachama wameweka maazimio muhimu yanayolenga kuimarisha usalama, utawala bora na utulivu wa kisiasa katika ukanda huo.
Katika hotuba yake ya kufunga kikao hicho, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mohamed Thabit Kombo, alisisitiza kuwa changamoto nyingi za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazoikumba Afrika haziwezi kutatuliwa kwa misaada ya nje bali kwa juhudi za Waafrika wenyewe.
"Hatuwezi kuendelea kutegemea wengine kutatua matatizo yetu,” alisema Kombo, akisisitiza dhima ya mataifa ya SADC kushughulikia migogoro ya ndani kwa njia za amani na majadiliano ya kina.
"Sheria na mifumo yetu ya ulinzi ni lazima ifanyiwe mapitio mara kwa mara"
Mkutano huo uliowaleta pamoja zaidi ya wajumbe 400 ulijadili kwa kina hali ya usalama katika ukanda wa SADC na kutathmini changamoto zinazokwamisha ustawi wa utawala bora.
Miongoni mwa maazimio yaliyopitishwa ni pamoja na: kutengeneza mifumo ya tahadhari za mapema ili kubaini viashiria vya hatari vya kisiasa, kukuza uwazi na uwajibikaji katika taasisi za serikali, na kuimarisha mifumo ya ulinzi wa uchaguzi huru na wa haki.
Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi, alisisitiza pia umuhimu wa kushughulikia uhalifu unaovuka mipaka kama vile usafirishaji haramu wa binadamu, dawa za kulevya, ujangili na uhalifu wa mtandao. "Sheria na mifumo yetu ya ulinzi ni lazima ifanyiwe mapitio mara kwa mara ili iweze kuhimili vitisho vipya vya usalama katika enzi ya kidijitali,” alisema Magosi.
Mzozo wa Kongo dabo unaendelea
Kikao hicho kimefanyika wakati hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ikizidi kuzorota, huku mgogoro kati ya serikali ya Kinshasa na waasi wa M23 ukiendelea.
Hata hivyo, Tanzania imetajwa kuwa mstari wa mbele katika juhudi za upatanisho, ikiwa ni sehemu ya majukumu yake kama mwenyekiti wa sasa wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC.
Katika hotuba yake ya awali ya ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Dkt. Samwel Shelukindo, alisisitiza umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa kikanda katika kujenga mifumo imara ya ulinzi, akisema: "Ni lazima tushirikiane kwa dhati kuzuia vitisho vya usalama vinavyovuka mipaka kabla havijaleta madhara.”
Tanzania inahudumu kama mwenyekiti wa asasi hiyo muhimu ya SADC kuanzia Agosti 2024 hadi Agosti 2025, nafasi iliyokabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa kilele wa SADC uliofanyika nchini Zimbabwe mwaka jana.
Kwa ujumla, mkutano huu wa ngazi ya juu umeweka msingi mpya wa ushirikiano wa kisiasa na usalama miongoni mwa nchi za SADC, huku matumaini yakielekezwa katika utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa kwa ajili ya kudumisha amani ya kudumu katika ukanda huo.