Rwanda yatajwa kutofautiana na mkuu wa AFC/ M23
4 Julai 2025Kulingana na ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa, lengo kuu la Rwanda ni unyonyaji wa rasilimali za Kongo huku wakieleza pia kuwa Rais Paul Kagame anayo dhamira ya kulitwaa kabisa eneo la mashariki mwa DRC ili kujipatia madini kwa wingi na bila malipo.
Lengo hilo la rais Kagame linakinzana na la kiongozi wa kundi la AFC/M23 Corneille Nangaa ambaye angependa kusonga mbele zaidi katika mapambano yake hadi mji mkuu Kinshasa na hivyo kumpindua Rais Félix Tshisekedi, jambo ambalo Rwanda inalipinga vikali, kwa mujibu wa wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa.
Taarifa zinaendelea kubaini kuwa Kigali imemuweka kando Corneille Nangaa katika suala zima la usimamizi wa vuguvugu hilo la waasi. Uasi wa M23 uliibuka tena mnamo Novemba mwaka 2021 na Corneille Nangaa alijiunga na vuguvugu hilo mnamo Desemba 2023, huku Muungano wa Mto Kongo (AFC) likiwa tawi lake la kisiasa.
Undani wa ripoti hiyo ya wataalamu wa UN
Wataalam wa Umoja wa Mataifa walibainisha mapema wiki hii kuwa Rwanda ilihusika moja kwa moja katika mzozo wa Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kwamba nchi hiyo ilikuwa na mamlaka na udhibiti kwa waasi wa M23.
Hii si mara ya kwanza kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa kueleza kuwa Rwanda inawaunga mkono waasi wa M23 katika vita vyao dhidi ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, FARDC, mashariki mwa DRC.
Lakini ripoti ya hivi majuzi ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa ilieleza bayana jukumu la Rwanda katika mzozo huo ikiwa ni pamoja na kupeleka idadi ya wanajeshi wanaokadiriwa kufikia 6,000, huku lengo ikiwa kujipatia ushawishi wa kisiasa na kulifikia eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini.Mara zote Rwanda imekuwa ikikanusha shutuma hizo.
Mitazamo ya wachambuzi wa siasa
Marius Mubalama, mchambuzi wa siasa za Kongo, anasema Umoja wa Mataifa unapaswa kuweka shinikizo zaidi kwa Rwanda ili iwaondoe wanajeshi wake nchini Kongo.
"Kuna azimio lililopitishwa kuitaka Rwanda kujiondoa mashariki mwa Kongo. Hii si mara ya kwanza kwa Rwanda kuivamia DRC na kukataa kujiondoa. Zaidi ya Azimio hilo nambari 2773, ambalo lilipitishwa kwa kauli moja, sasa inatakiwa kuwepo utaratibu na mifumo itakayopelekea Rwanda kuhisi shinikizo. Vinginevyo watakaa na kuendelea kunyonya rasilimali za madini."
Ikumbukwe hata hivyo kuwa Rwanda ilitia saini mkataba wa amani na DRC wiki iliyopita mjini Washington. Lakini wachambuzi wa siasa wanairai mamlaka ya Kongo kuwa waangalifu, wakidai kuwa mara kadhaa Rwanda imeonekana kutoheshimu ahadi inazozitoa.
Kulingana na mchambuzi wa siasa za Maziwa Makuu Boniface Musavuli, maslahi ya kiuchumi yanayohusishwa na rasilimali za madini huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yanazuia mwitikio wowote thabiti kutoka kwa jamii ya kimataifa hasa mataifa ya Magharibi ambayo ndio wanufaika wakubwa.