Rwanda yapitisha sheria kali kuyadhibiti makanisa
12 Machi 2025Kanuni hizi pia zinasema kwamba ili mtu aruhusiwe kufungua nyumba ya ibada au kanisa, atatakiwa kulipa pesa milioni mbili faranga za Rwanda ambazo ni sawa na dola za Marekani elfu moja na mia sita.
Pia kwa mujibu wa kanuni hizi mpya mtu atakayefungua kanisa au nyumba ya ibada atatakiwa kuwa na elimu ngazi ya Chuo Kikuu katika masomo ya theolojia au mafunzo ya dini.
Lakini kama hilo halitoshi nyumba ya ibada au kanisa itatakiwa kuonyesha mfumo mzima wa uongozi wake na wajibu wa kila mtu lakini pia kuonyesha jinsi mapato yanavyoingia kanisani.
Zaidi lakini huyu atakayehitaji kufungua kanisa au nyumba ya ibada atatakiwa kuonyesha ramani ya jengo la ibada kuhakikisha ikiwa kweli linakidhi viwango vya kuitwa nyumba ya ibada au kanisa.
Je, ni haki kwa serikali kuingilia kati nyumba za ibada ?
Kanuni hizi zimetolewa na bodi ya taifa ya utawala ambayo kwa kawaida huratibu utendaji kazi wa taasisi mbalimbali za utawala na mashirika yasiyo ya kiserikali.
Mkurugenzi wake mkuu Dr Doris Uwicyeza Picard anasema baada ya uchunguzi uliofanywa na serikali kulionekana matatizo mengi kuhusu utendaji kazi wa makanisa na nyumba za ibada kuhusu usajili na pesa inayoingia.
"Ni pesa yenu ambayo mnakuwa mmeitoa lakini hamjui pesa hiyo inakwenda wapi, hata sasa ninapozungumza michango inaendelea na ujenzi wa hapa na pale makani lakini ngoja niwaulize hivi mnajuaje ikiwa kweli pesa mnayoitoa inakwenda kujenga kanisa hilo ?", alihoji Uwicyeza kabla ya kuongeza :
"Wakati mwingine mnatoa pesa kiasi kikubwa kupitia michango ya pamoja kila wiki kwamba wajenge kanisa, lakini mnajuaje ikiwa hata kama kanisa hilo likijengwa litakuwa limesajiliwa kama mali ya waumini siyo mali binafsi ya mchungaji na mmiliki wa kanisa hilo."
"Hata Mungu anawapenda watu wenye akili"
Dr Doris Uwicyeza Picard anasema makanisa lazima yawe na akaunti za benki.
"Watu wanatoa sadaka kila siku na sadaka hii inapokelewa mikononi mwa watu lakini huwezi kujua wala kuelewa ni wapi pesa inayotokana na sadaka hii inaishia katika mikono ya nani.Sisi tunahitaji makanisa yenye akaunti benki kiasi kwamba mkipata pesa hiyo peleka benki", alisisitiza.
Hata hivyo uamuzi huu umezua minong'ono baadhi wakidai kuwa uamuzi huu wa serikali unanuia kudhoofisha shughuli za ibada huku wengine wakionekana kuridhia uamuzi huo. Floribert Kabera ni muumini wa kikristo mjini Kigali.
"Tunaamini kuwa Mungu hutoa hekima na akili kwa watumishi wake lakini kwa sasa elimu ya dini ni muhimu,maana hapo awali kulikuwa na tatizo la watu kufungua nyumba za ibada na makanisa kiholelaholela kiasi kwamba hata watu wasiojua kusoma wala kuandika walikuwa wakiamka asubuhi anafungua kituo cha kusalia na mwisho linakuwa kanisa la ibada, kwa hiyo kusoma siyo vibaya maana hata Mungu anawapenda watu wenye akili."
Sheikh Sindayigaya Musa Mufti mkuu wa Rwanda anasema huenda sasa kanuni mpya zikapuguza kasi ya kufungua makanisa au nyumba mpya za ibada.
"Kama mtu atafungua kanisa au nyumba ya ibada na akatakiwa kuwa na sahihi za watu 1000 maana yake ni ushahidi kuwa ama kanisa hili linahiajika katika eneo hilo au la, na hii itasaidia kuepuka kujenga hilo na mwisho usiwe na waumini wa kuhudhuria huduma za kiroho."
Shinikizo la rais Kagame bungeni
Miezi miwili iliyopita rais Paul Kagame akizungumza bungeni aliwaomba wabunge kutathmini na kuona sheria zinalishughulikiaje tatizo hili akisema kwamba kukosekana kwa muongozo muhimu wa uratibu wa shughuli za ibada kulisababisha jamii kuwa katika hali isiyoeleweka.
"Hayo makanisa au nyumba za ibada na viongozi kwa kawaida wana sheria zinazopaswa kuratibu shughuli zao lakini imekuwaje hadi tufike hapa? Ninyi kama wabunge au hata wananchi wengine hata hizo sheria kama hazitoshi basi zitazamwe upya", alisema Kagame.
Kufuatia kauli hiyo wadadisi wanahisi hilo lilikuwa ni agizo na si hoja ya kawaida. Shughuli za kufunga makanisa na nyumba za ibada zilianza mwezi wa nane mwaka 2024 na wakati huo makanisa na nyumba za ibada elfu tisa mia nane zilifungwa.
Sasa wakati kanuni hizi mpya zikitangazwa makanisa na nyumba za ibada mia sita zimetajwa kufutwa kabisa kutoka orodha ya zile zinazoendelea kuomba kufunguliwa tena baada ya kukidhi viwango vinavyotakiwa.