Rwanda yajiunga na ukosoaji wa utawala mbadala wa M23
29 Mei 2025Mataifa 12 ya Afrika, yakiwemo Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), yamelaani vikali hatua ya kundi la waasi la M23 kuanzisha "utawala mbadala" katika maeneo waliyotekwa mashariki mwa DRC.
Taarifa ya pamoja iliyosainiwa katika mkutano wa kikanda mjini Entebbe, Uganda, inalaani pia ushawishi wa muungano wa waasi wa Congo River Alliance (AFC) ambao M23 ni sehemu yake.
Rwanda, licha ya kuwa miongoni mwa wanaotuhumiwa kulisaidia kundi la M23 kwa silaha na ushauri wa kijeshi, ilitia saini taarifa hiyo – hatua ambayo wachambuzi wa kisiasa wanaiona kama ishara ya Kigali kuanza kutathmini gharama ya kidiplomasia na kifedha ya msaada wake kwa waasi.
Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu kama Amnesty International wameishtumu M23 kwa mauaji ya kiholela, mateso na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, hasa dhidi ya raia waliokamatwa kinyume cha sheria.
M23 imekanusha tuhuma hizi, lakini picha ya jumla inazidi kuwa tata huku mashirika ya misaada yakisema idadi halisi ya waathirika inaweza kuwa kubwa kuliko inavyoripotiwa.
Uamuzi wa Rwanda kusaini taarifa ya kulaani kundi hilo linaloonekana kuwa mshirika wake ni hatua muhimu, hasa wakati ambapo mashinikizo kutoka mataifa ya Magharibi kama Ubelgiji yanaongezeka.
Katika hatua nyingine, taarifa ya Entebbe imetoa wito kwa makundi yote ya kigeni yenye silaha mashariki mwa DRC – likiwemo kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), Allied Democratic Forces (ADF), CODECO na RED-Tabara – kusalimisha silaha bila masharti.
FDLR, linalojumuisha wahalifu wa mauaji ya kimbari ya 1994 nchini Rwanda, linatajwa na M23 kama sababu ya kuanzisha mashambulizi yake, huku serikali ya Kinshasa ikituhumiwa kulifadhili kundi hilo.
Joseph Kabila aripotiwa Goma: Kisigino kwa juhudi za amani
Katika hali inayochochea mvutano zaidi, rais wa zamani wa Congo, Joseph Kabila, ameripotiwa kuwasili Goma – mji ulio chini ya udhibiti wa waasi wa M23 tangu Januari – kwa ajili ya mashauriano na wananchi.
Vyanzo vitatu vya karibu naye vimeiambia Reuters kuwa Kabila alifika Jumapili usiku na anatarajiwa kuanza vikao vya hadhara.
Kabila hajatoa tamko lolote kuhusu ziara hiyo, lakini kiongozi wa muungano wa waasi Corneille Nangaa amedokeza uwepo wake kupitia mitandao ya kijamii.
Kabila anakabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kibinadamu na uungwaji mkono wa uasi wa M23, na wiki iliyopita Seneti ya Congo ilipiga kura ya kumvua kinga ya kisheria. Serikali imesitisha shughuli za chama chake na kuanza kukamata mali za viongozi wake.
Msemaji wa serikali Patrick Muyaya alisema kupitia televisheni ya taifa kuwa "Kabila sasa anajitokeza wazi kama kiongozi wa waasi pamoja na Rais Paul Kagame wa Rwanda."
Kulingana na mshauri mkuu wa Rais Donald Trump kuhusu masuala ya Afrika, Massad Boulos, Marekani inasukuma kufikiwa kwa mkataba wa amani katika msimu huu wa kiangazi, sambamba na mikataba ya uchimbaji wa madini inayolenga kuleta uwekezaji mkubwa wa Magharibi katika eneo hilo.
Hata hivyo, hali ya kutoaminiana kati ya Kinshasa na Kigali inazidi kuwa kikwazo kikubwa. Rwanda inakana kuhusika moja kwa moja na M23, ikisema ina haki ya kujilinda dhidi ya vitisho vya kijeshi kutoka Congo na makundi kama FDLR.
Umoja wa Mataifa na mataifa ya Magharibi, hata hivyo, yanaendelea kudai ushahidi wa usaidizi wa Rwanda kwa M23 ni thabiti na unaendelea.
Vyanzo: RTRE, DPAE