Rwanda yaishutumu Uingereza kwa kusitisha msaada wa kifedha
26 Februari 2025Rwanda imeitaja Uingereza kama ambayo sasa imeonyesha inasimama upande gani katika mzozo wa DRC na ikaongeza kwamba daima haitakubali kuweka rehani usalama na maisha ya raia wake kwa kuogopa vikwazo. Kutoka Kigali mwandishi wetu Sylivanus Karemera anaripoti zaidi.
Vikwazo vilivyotangazwa na Uingereza ni pamoja na kusitisha kwa muda misaada ya fedha ya moja kwa moja kwa serikali ya Rwanda isipokuwa misaada kwa watu maskini na wenye mahitaji maalum, kuzuia matangazo ya kuitangaza Rwanda katika medani za kimataifa, kusitisha ushirikiano katika mafunzo ya kijeshi baina ya nchi mbili pamoja na kususia kuhudhuria mikutano ya kimataifa inayofanyika Rwanda. Uingereza imesema pia kwamba itaendelea kushirikiana na mataifa mengine kutathmini uwezekano wa kuiwekea vikwazo zaidi Rwanda. Uingereza pia imechukua uamuzi huo kama njia ya kuiwajibisha Rwanda kutokana na kuhusika kwake katika mzozo wa Congo.
Kupitia tangazo lake serikali ya Rwanda imesema wazi kwamba vikwazo vya Uingerereza dhidi yake sasa vinaiweka Uingereza katika nafasi yake kwenye mzozo huu na kwamba Rwanda inasikitishwa na uamuzi huo wa Uingereza.
Rwanda imesema kwamba haingii akilini Uingereza kudhani kwamba Rwanda itautelekeza usalama wa raia wake kwa sababu ya kuogopa vikwazo.
Tangazo la serikali ya Rwanda linasema kwamba kamwe Rwanda haiwezi kuvishwa mzigo wa uongozi mbovu wa serikali ya Kinshasa huku mataifa makubwa yakiendelea kuibembeleza kwa sababu ya maslahi yanayojulikana.
Kutangazwa kwa vikwazo hivi kumezua malalamiko kutoka kwa wananchi wa kada zote hasa kwenye mitandao ya kijamii, lakini pia wanasiasa wamelaani kitendo hicho. Dr Frank Habineza ni mkuu wa chama cha Green Party of Rwanda "M23 ni raia wa Kongo siyo wa Rwanda, hawa ni watu waliojikuta pale baada ya mipaka kuchorwa na wakoloni hilo ni jambo la wazi hata DRC inalitambua ni watu wanaopambana kwa ajili ya kudai haki zao. Inakuwaje kila mara serikali ya DRC inailaumu Rwanda? Sisi tunaitaka serikali ya DRC iwasikilize watu wake na siyo kutulaumu sisi"
Bi Christine Mukabunani ni mkuu wa chama cha PS-Imberakuri anasema linapokuja suala la maslahi mapana ya nchi wao kama wanasiasa tofauti zao wanaziweka kando "Linapokuja suala la kulinda maslahi ya nchi yetu sote tunasimama pamoja, hapa hakuna cha mimi ni wa chama gani hapana na ndiyo maana tumetoa wito kwa kila mtu kuitetea nchi hii hatutakubali hii ni vita ya wananchi wote."
Vikwazo vya Uingereza vimekuja wiki moja baada ya Marekani kumuwekea vikwazo naibu waziri wa mashauri ya kigeni anayehusika na ushirikiano wa kikanda jenerali mstaafu James Kabarebe. Yeye ameliambia bunge jana jioni kwamba mataifa yote yanayoweka vitisho vya vikwazo wao ndiyo walipaswa kuwajibika pamoja na serikali ya Kinshasa ambaye yeye anasema ndiyo cha mzozo huu. "Wote wanawajibika, ukiona mataifa makubwa yakijitoatoa kutangaza vikwazo, wao ndiyo wanapaswa kuwekewa vikwazo kwanza, watu wa mwanzo kabisa ambao wangewekewa vikwazo katika mzozo wa mashariki mwa DRC ni jamii ya kimataifa."
Uingereza imekuwa mshirika mkubwa wa Rwanda baada ya Marekani hasa katika nyanja za ulinzi na usalama, elimu, kilimo, utawala bora na mazingira. Vikwazo hivi vya Uingereza huenda vikaathiri mikataba ya kati ya serikali ya Rwanda na timu ya arsenal kuhusu kuitangaza Rwanda lakini pia kuathiri pesa katika sekta ya kiuchumi na uwekezaji kwa ujumla.