Rwanda yaikosoa HRW kuhusu ongezeko la makaburi
5 Septemba 2025Human Rights Watch ilisema jana kwamba, makaburi 460 yaliongezwa kati ya Disemba 15 na Julai 3, huku picha za satelaiti zikionyesha jumla ya makaburi mapya 1,171 tangu mwaka 2022.
Ripoti hiyo inahusisha ongezeko hilo na operesheni za kijeshi zinazodaiwa kuhusisha wanajeshi wa Rwanda na kundi la waasi la M23 mashariki mwa DRC.
Picha zilizochapishwa na shirika hilo kupitia mtandao wa kijamii wa X, zinaonyesha mabadiliko katika makaburi hayo ya kijeshi tangu mapema mwaka 2022, ikiwemo kuongezwa kwa makaburi mapya 1,171.
Rwanda imesisitiza kuwa wanajeshi wake waliouawa hawazidi 10, ikikanusha madai ya kuhusika moja kwa moja na mzozo huo.
Ripoti hiyo imekosolewa vikali na msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo ambaye ameitaja ripoti hiyo kwamba haina ukweli wowote na kwamba shirika hilo "linatafuta umaarufu kwa nguvu."
Ripoti hiyo ya HRW imeibua mjadala kuhusu ushiriki wa Rwanda katika mzozo wa Kongo, huku gazeti la Uingereza la The Guardian likiwa la kwanza kuripoti kuhusu ongezeko la makaburi hayo mnamo Februari.