Rwanda yaandaa Mkutano wa 20 wa Maaskofu barani Afrika
1 Agosti 2025Mkutano huu unafanyika wakati ambapo eneo la Maziwa Makuu, hususan Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo linaendelea kukumbwa na mizozo ya kivita. Maaskofu wameitumia fursa hii kutoa mwito wa amani na maridhiano.
Mkutano huu unafanyika chini ya kauli mbiu: "Yesu Kristo ndiye Mwanzo wa Matumaini, Maridhiano na Amani."
Kauli hii imeakisi mijadala ya ufunguzi ambapo viongozi wengi wa Kanisa wametoa wito wa kuwepo kwa maelewano, uvumilivu, mshikamano na amani miongoni mwa Waafrika, wakimtaja Kristo kama kiungo kikuu cha uvumilivu huo.
Padre Chesco Peter Msaga, Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania, ameeleza kwa kina kiini cha mkutano huo unaofanyika Kigali.
"Maaskofu wamekuja kwa pamoja hapa kwanza ili kuonyesha mshikamano wao lakini vilevile ili kujifunza kwa karibu kuona ni mambo gani msingi yanaweza kufanyika ili kuleta amani katika mazingira yetu na hasa katika kanda ya maziwa makuu. Tunatambua kwamba bado kuna maeneo ambayo yana vita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pamoja na kwamba tunatambua kwamba kuna makubaliano ya amani ambayo yanaendelea lakini bado kuna migogoro inayoendelea."
Maelewano na mshikamano miongoni mwa Waafrika
Kadinali Fridolin Ambongo, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Mwenyekiti wa SECAM amesema viongozi wa Kanisa hawawezi kunyamaza wakati ambapo dunia inakumbwa na changamoto kubwa.
"Tumeitwa kuchukua hatua kwa ajili ya kuleta amani, na kuwa nyenzo muhimu ya suluhu. Huu si mwito wa kitheolojia tu, bali pia ni dharura ya kitume. Kanisa Barani Afrika linapaswa kuwa alama ya umoja, haki, maridhiano na amani, ili tuweze kusimama pamoja katika muungano—hasa katika nchi kama hii ya Rwanda ambayo ni kielelezo kuwa maridhiano yanawezekana."
Viongozi hao wamesema Kanisa haliwezi kusalia kimya wakati dunia ikikabiliwa na misukosuko ya kiusalama, siasa za chuki, na migogoro ya kijamii.
Askofu Arnaldo Sanchez Catalan, Mwakilishi wa Papa Mtakatifu nchini Rwanda, alitaja mzozo unaoendelea kati ya Rwanda na DRC kama mfano wa hali inayohitaji jitihada za pamoja za kuleta amani.
"Amani ni kiungo muhimu katika kutafuta matumaini. Katika muktadha huu, SECAM inakutana Kigali kutafakari jinsi Kanisa Katoliki linavyoweza kushiriki kikamilifu katika kutafuta amani, kustahimili baada ya mizozo na kupona kabisa."
Mkutano huu wa 20 unahudhuriwa na zaidi ya maaskofu 250 kutoka nchi mbalimbali za Afrika. Baada ya mijadala, wataandaa ripoti ya maazimio ya pamoja kuhusu mchango wa Kanisa Katoliki katika kustawisha jamii na kuimarisha ustahimilivu wa kijamii barani Afrika.