Rwanda kuwapokea wahamiaji 250 kutoka Marekani
5 Agosti 2025Wakifika Rwanda watakuwa na haki ya kuishi katika nchi hiyo, kurudishwa katika nchi walikotoka kwa hiari au kupelekwa katika nchi ya tatu.
Mpango wa kuwapeleka nchini Rwanda wahamiaji hao kutoka Marekani awali ulisikika katika mitandao ya kijamii mwezi Juni mwaka huu na wakati huo ilisemekana kwamba nchi hizo mbili zilikuwa tayari zimetia saini mkataba wa kutekeleza zoezi hilo.
Wakati huo Rwanda ilipokea orodha ya majina ya watu kumi ambao watakuwa ni kundi la kwanza kupelekwa Rwanda, ambao hata hivyo haikujulikana uraia wao.
Sasa Msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo akizungumza na shirika la habari la Reuters amethibitisha hatua hiyo ya Rwanda kuwapokea wahamiaji hao.
"Rwanda imekubaliana na Marekani kuwapokea hadi wahamiaji 250, kwa sababu kwa sehemu moja karibu kila familia nchini Rwanda inatambua ugumu na athari za ukimbizi na tunu zetu zimejengwa kwa misingi hiyo ya kurekebisha watu na kuwarudisha katika jamii wakiwa ni watu bora zaidi” amesema afisa huyo.
Mkataba waipa Rwanda haki ya kuchagua wahamiaji
Kupitia mkataba huu Rwanda itakuwa na uwezo wa kuchunguza na kujiridhisha na kila mhamiaji aliyependekezwa kupelekwa Rwanda ili kuona ikiwa anakidhi vigezo vilivyoainishwa na kukubaliana katika mkataba huo.
Wale watakaopokewa Rwanda watakuwa na haki ya kupewa mafunzo ya muda mfupi, huduma za afya, na makazi ili kuwaruhusu kuanza maisha mapya nchini Rwanda au baadaye kupelekwa katika nchi ya tatu.
Rwanda inaamini kwa kufanya hivyo itakuwa imechangia katika huduma bora kwa binadamu lakini pia kupitia watu ambao baadhi yao wana ufundi na maarifa ya kiwango cha juu itanufaika na ujuzi huo na hivyo kuchangia maendeleo ya nchi hiyo.
Utawala wa Rais wa Marekani Donald Trump umeapa kuwahamisha Marekani mamilioni ya wahamiaji haramu wa nchi za kigeni waishio katika nchi hiyo kinyume cha sheria, wale waliofanaya makosa ya jinai au hata wale waliokamilisha adhabu zao magerezani hadi katika nchi za kigeni kama vile Sudan Kusini na Eswatin au Swaziland.
Hata hivyo wachambuzi wa kimataifa wamekosoa mpango huo wa Rais Trump kama hatua ya kuhatarisha maisha ya wahamiaji hao kwa sababu huenda hata wakarudishwa katika nchi zao walizokimbia kwenda Marekani.
Kupitia mpango huu Marekani itakuwa tayari kutoa misaada ya kifedha kwa Rwanda kiasi ambacho hata hivyo hakijawekwa wazi kwa kila mmoja kufahamu.
Ni mkakati ambao unafuatia ule ambao ulikuwepo baina ya Rwanda na Uingereza ambao ulishindwa kutekelezwa kufuatia kujiondoa kwa serikali ya waziri mkuu wa sasa wa Uingereza Keir Starmer