Rwanda na Kongo kuanzisha ushirikiano wa kiuchumi
2 Agosti 2025Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ni kwamba Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siku ya Ijumaa (01.08.2025) zimekubaliana juu ya ushirikiano jumuishi wa kiuchumi wa kikanda. Huku nchi hizo mbili zikichukua hatua kuelekea utekelezaji wa makubaliano ya amani yaliyosainiwa mjini Washington mwezi Juni.
Hati iliyokubaliwa Ijumaa baina ya nchi mbili hizo inajumuisha ushirikiano katika sekta za nishati, miundombinu, minyororo ya usambazaji wa madini, hifadhi za kitaifa na afya ya umma.
Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walisaini makubaliano ya amani mwezi Juni mjini Washington, katika mazungumzo yaliyoandaliwa na Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, ambayo yalilenga kumaliza mapigano yaliyosababisha vifo vya maelfu na kuvutia uwekezaji wa mabilioni ya dola kutoka Magharibi kwenye eneo lenye utajiri wa madini kama tantalum, dhahabu, cobalt, shaba, lithium na mengineyo.
Kama sehemu ya makubaliano hayo, Kinshasa na Kigali walikubaliana kuzindua mfumo wa ujumuishaji wa kiuchumi wa kikanda ndani ya siku 90, kwa mujibu wa mkataba huo.
Chanzo kinachofahamu suala hilo kilisema rasimu ya awali ya makubaliano hayo tayari imekubaliwa, na sasa kutakuwa na kipindi cha kupokea maoni kutoka sekta binafsi na asasi za kiraia kabla ya mkataba huo kukamilishwa.
Udhibiti kamili wa rasilimali za kitaifa?
Makubaliano hayo yanapangwa kusainiwa kwenye mkutano wa wakuu wa nchi utakaofanyika Ikulu ya Marekani. Hata hivyo tarehe ya mkutano huo bado haijapangwa.
Katika taarifa ya Ijumaa, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walithibitisha kuwa kila nchi ina "udhibiti kamili na wa kizalendo” juu ya uchimbaji, usindikaji na usafirishaji wa rasilimali zake za asili, na walitambua umuhimu wa kukuza uwezo wa usindikaji na uongezaji thamani wa madini ndani ya kila nchi, kwa mujibu wa nakala iliyoonwa na shirika la habari la Reuters.
Kinshasa inaona uporaji wa utajiri wake wa madini kuwa chanzo kikuu cha mgogoro kati ya jeshi lake na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda mashariki mwa DRC.
Shirika la Reuters liliripoti mwezi Mei kwamba madini ya Kongo kama tungsten, tantalum na bati—ambayo Kinshasa kwa muda mrefu imeishutumu Rwanda kwa kuyanyonya kinyume cha sheria—yanaweza kuuzwa kihalali kwenda Rwanda kwa ajili ya usindikaji chini ya masharti ya mkataba unaojadiliwa na Marekani.
Nchi hizo mbili zimejitolea kuhakikisha kuwa biashara ya madini haitumiki tena kufadhili makundi ya waasi, na kujenga sekta ya madini ya viwanda ya hali ya juu katika ukanda huo, pamoja na kuhakikisha ufanisi wa kuvuka mipaka katika minyororo ya usambazaji wa madini, kwa mujibu wa taarifa hiyo.
Miundombinu mipya
Pia walikubaliana kuunganisha miundombinu mipya kwenye ushoroba wa Lobito mradi unaoungwa mkono na Marekani, jambo linaloonesha nia ya Washington ya kupata fursa zaidi za rasilimali katika eneo hilo na kupambana na ushawishi wa China.
Miradi pekee iliyotajwa kwenye taarifa hiyo ni mradi wa umeme wa Ruzizi III na uchimbaji wa gesi ya methane kutoka Ziwa Kivu, licha ya Marekani kusisitiza umuhimu wa madini adimu. Nchi hizo zilisema wanakusudia kuweka kipaumbele kwa ufadhili wa bwawa la umeme la Ruzizi na kushirikiana kwa karibu katika uchimbaji endelevu wa gesi ya methane.
Tangazo la Ijumaa linakuja baada ya nchi hizo mbili kufanya mkutano wa kwanza wa kamati ya pamoja ya ufuatiliaji siku ya Alhamisi kama hatua ya kuelekea utekelezaji wa makubaliano ya amani ya Washington, ingawa bado kuna ahadi nyingine ambazo hazijatimizwa.
Ahadi za makubaliano ya amani ya Washington
Katika makubaliano ya Washington, nchi hizo mbili za Afrika ziliahidi kutekeleza mkataba wa mwaka 2024 ambao unahusisha kuondolewa kwa wanajeshi wa Rwanda mashariki mwa Kongo ndani ya siku 90.
Operesheni za kijeshi za jeshi la Kongo dhidi ya waasi wa Rwanda wa FDLR, (kundi la waasi lenye makao yake mashariki mwa Congo linalojumuisha mabaki ya jeshi la zamani la Rwanda na wanamgambo waliotekeleza mauaji ya kimbari ya 1994), zinapaswa pia kukamilika ndani ya kipindi hicho hicho.
Makubaliano hayo pia yalisema Kongo na Rwanda zitaunda mfumo wa pamoja wa uratibu wa usalama ndani ya siku 30 na kutekeleza mpango ulioafikiwa mwaka jana wa kufuatilia na kuthibitisha kuondoka kwa wanajeshi wa Rwanda ndani ya miezi mitatu.
Lakini siku 30 tangu kusainiwa kwa makubaliano hayo zimepita bila kikao cha mfumo wa uratibu wa usalama kufanyika.
Chanzo kinachofahamu suala hilo kilisema kikao cha mfumo huo wa pamoja wa usalama kimepangwa kufanyika tarehe 7 Agosti huko Addis Ababa.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo pia inashiriki mazungumzo ya moja kwa moja na M23 yanayoandaliwa na Qatar, na mwezi uliopita pande hizo mbili zilikubaliana kusaini mkataba mwingine wa amani ifikapo Agosti 18, ingawa kuna mambo mengi bado yanayohitaji majadiliano.