Rwanda, DRC zasaini makubaliano ya amani Marekani
27 Juni 2025Katika hafla iliyofanyika Ijumaa mjini Washington, Rwanda na DR Kongo zilitia saini makubaliano ya amani yenye lengo la kumaliza mapigano yaliyoangamiza maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni kuyakimbia makazi yao. Makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Marekani, Qatar na Umoja wa Afrika, yameahidiwa kuwa mwanzo wa ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, aliyeshuhudia utiaji saini huo, alisema ingawa bado kuna kazi kubwa mbele, mkataba huu unatoa matumaini mapya kwa watu wa eneo hilo. "Sasa watu wanaweza kuanza kuota ndoto mpya za maisha bora," alisema Rubio.
Mkataba huu umefuatia kuibuka upya kwa waasi wa M23 - kundi la waasi wa Kitutsi linalohusishwa kwa karibu na Rwanda—ambalo lilifanikiwa kuteka maeneo makubwa mashariki mwa DRC, yakiwemo jiji muhimu la Goma. Ingawa mkataba haukutaja moja kwa moja mafanikio ya M23, unaitaka Rwanda kusitisha kile kilichotajwa kama "hatua za kujihami.”
Rwanda imekana kuunga mkono M23 moja kwa moja lakini imekuwa ikisisitiza haja ya kuondolewa kwa kundi lingine la waasi—FDLR—lililoundwa na Wahutu waliotuhumiwa kuhusika na mauaji ya halaiki ya Watutsi nchini Rwanda mwaka 1994. Makubaliano hayo yanasisitiza kuwa FDLR lazima "wafifishwe kwa njia ya kijeshi.”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, alisema hatua ya kwanza ni kutekeleza mpango wa kuondoa kabisa FDLR, pamoja na kusitisha hatua za Rwanda za kujihami. Alisema hatua hiyo inathibitisha dhamira ya kweli ya kusitisha msaada wa kiserikali kwa makundi ya waasi.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba Wagner, alisisitiza umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya kitaifa na sheria za kimataifa. "Kwa kusaini makubaliano haya, tunathibitisha ukweli mmoja rahisi: amani ni chaguo lakini pia ni wajibu wa kulinda sheria za kimataifa na uhuru wa mataifa," alisema.
Mzozo wa rasilimali, siasa za kimataifa na maoni tofauti
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo pia ni Massad Boulos, mfanyabiashara mwenye asili ya Lebanon na mshauri maalum wa Rais Donald Trump kuhusu Afrika. Alieleza kuwa mkataba huo utaanzisha chombo cha pamoja cha uratibu wa usalama kitakachosaidia kurejesha wakimbizi katika maeneo yao ya asili.
Rais Trump alijitokeza hadharani kusifu juhudi zake katika kufanikisha makubaliano hayo na kulalamikia kutopokea Tuzo ya Amani ya Nobel, akidai kwamba Marekani sasa itafaidika na haki za uchimbaji wa madini kutoka Kongo. "Tutapata haki nyingi za madini kutoka Kongo," alisema Trump, akisisitiza umuhimu wa madini kama lithium na cobalt kwa teknolojia ya magari ya umeme—sekta ambayo China tayari imejikita sana.
Katika maelezo ya kushangaza, Trump alikiri kutofahamu kwa kina historia ya mzozo wa DRC na Rwanda, lakini akarejelea machungu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 akisema: "Nilichojua tu ni kwamba walikuwa wanapigana kwa miaka mingi kwa kutumia mapanga."
Lakini siyo kila mtu alishangilia mkataba huo. Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake Denis Mukwege—mshindi mwenza wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2018 kwa juhudi zake dhidi ya ukatili wa kingono katika vita vya DRC—alitangaza wasiwasi wake. Kwa mujibu wa Mukwege, mkataba huu unazipa Rwanda na Marekani faida kubwa huku ukiyadhoofisha madai ya haki kwa waathiriwa wa uvamizi na uporaji wa rasilimali.
"Mkataba huu ni kama zawadi kwa uvamizi, unahalalisha uporaji wa rasilimali za Kongo, na unamlazimisha mhanga kuuza urithi wake wa kitaifa kwa matumaini ya amani tete na ya muda mfupi," alisema Mukwege.
Wakati huo huo, nchi zote mbili zinaonekana kujitahidi kupata uhusiano wa karibu na Marekani. DRC imependekeza mkataba wa madini unaofanana na ule ambao Marekani iliingia na Ukraine wakati wa utawala wa Trump. Rwanda nayo imekuwa ikijadili makubaliano ya kuwahifadhi wahamiaji wanaofukuzwa Marekani—kipaumbele kikubwa kwa Trump.
Ingawa Rwanda inasifiwa kuwa moja ya mataifa tulivu zaidi Afrika, mpango wake wa awali wa kushughulikia wahamiaji waliokuwa wafukuzwe Uingereza ulifutwa baada ya mabadiliko ya uongozi nchini humo mwaka jana.
Wakati mkataba huu wa Washington unatajwa kuwa hatua kubwa kuelekea amani ya kudumu kati ya DRC na Rwanda, baadhi ya wachambuzi wanaonya kuwa mafanikio yake hayatategemea tu nia njema ya kisiasa, bali pia uwazi wa utekelezaji wake, usawa wa kiuchumi na ushirikishaji wa waathiriwa wa mzozo. Swali linalosalia: Je, ni kweli amani inaweza kununuliwa kwa bei ya madini?