Rutte: Urusi inasalia kuwa tishio kubwa kwa NATO
4 Aprili 2025Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa mawaziri wa NATO mjini Brussels, Rutte amesema jukumu la kusitisha vita nchini Ukraine liko mikononi mwa Urusi.
"Ni wazi, sasa mpira uko mikononi mwa Urusi, kwa hivyo lazima tuone nini kitatokea. Lakini sitaki kuingilia mazungumzo hayo kwa kutoa maoni yangu. Tutaona jinsi itakavyokuwa."
"Hadi sasa, lazima niseme, nimefurahishwa sana na jinsi Marekani inavyoendesha mazungumzo hayo na wakati ikiihusisha Ulaya na Ukraine. Washirika wa Ulaya wanafuatilia na kujulishwa kinachotokea. Alisema Rutte.
Soma pia: Mawaziri wa NATO wajadili mustakabali wa Ukraine
Katika mkutano huo baadhi ya mawaziri wa Umoja wa Ulaya wametaka Moscow iwekewe tarehe ya mwisho, kujibu pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano, lakini Rutte alikataa kubainisha kwamba anaunga mkono pendekezo hilo.
Rutte ameendelea kusema kwamba wanachama wa jumuiya hiyo watatumia fedha zaidi katika ulinzi, na washirika wengi tayari wameanza kufanya hivyo.
Alipoulizwa kuhusu ushuru mpya wa Marekani uliotangazwa na Rais Donald Trump, Katibu Mkuu huyo wa NATO aliwaambia waandishi wa habari kuwa haukiuki mikataba ya Muungano huo wa Kijeshi.