Ruto akwepa kuzungumzia maandamano Kenya
8 Julai 2025Katika tukio la hadhi ya kimataifa lililofanyika katika Ikulu ya Nairobi Rais Ruto alikutana na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, pamoja na Rais wa Senegal, Macky Sall, katika uzinduzi wa makao makuu mapya ya Kituo cha Kimataifa cha Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi. Licha ya hali tete iliyoikumba nchi siku ya Jumatatu, Rais Ruto hakuonyesha dalili yoyote ya kuguswa na maelfu ya raia waliokuwa mitaani wakilalamikia gharama ya juu ya maisha, ukandamizaji wa polisi na kupuuza kwa sauti ya umma.
Watu wanne wameuawa nchini Kenya
Wakati taifa likiwa bado linaomboleza vifo na majeruhi vilivyotokea miongoni mwa waandamanaji, hotuba ya Rais haikutaja tukio hilo la jana. Badala yake, Rais alielekeza nguvu zake kwenye mazungumzo ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi, akisisitiza kuwa Afrika ni “chimbuko la suluhisho la tabianchi” na kuhimiza jamii ya kimataifa kuwekeza zaidi katika juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
“Kuanzishwa kwa makao makuu mapya ya Kituo cha Kimataifa cha Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi jijini Nairobi, ni ishara muhimu kwamba masuala ya mabadiliko ya tabianchi, yanastahili kupewa uzito kote ulimwenguni,” alisema rais Ruto.
Licha ya uzito wa ajenda ya mazingira, ukimya wa Rais kuhusu yaliyotokea jana umetafsiriwa na baadhi ya wachambuzi wa siasa kama dhihirisho la kupuuza kilio cha wananchi walioteswa na vyombo vya dola. Taarifa rasmi kutoka kwa Huduma ya Kitaifa ya Polisi ilithibitisha vifo vya watu 11, kukamatwa kwa zaidi ya watu 500, na kujeruhiwa kwa raia na maafisa wa usalama katika makabiliano makali yaliyoambatana na uporaji na uharibifu wa mali. Chekai Musa ni mchambuzi wa masuala ya siasa.
Hali ni tete mjini Nairobi huku vijana wakiendelea kushiriki maandamano ya kuipinga serikali
Wakati hali bado ni tete na miito ya uwajibikaji ikiongezeka, bado haijajulikana ni lini Rais Ruto atatoa kauli rasmi kuhusu hali ya usalama nchini, vifo vya raia na madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu. Lakini je Wakenya wanahisi vipi?
Kwa sasa, picha ya Rais akisimama bega kwa bega na Ban Ki-moon na Macky Sall inasalia kuwa ya mwelekeo wa kidiplomasia, lakini yenye ukakasi mkubwa kwa wananchi waliopoteza wapendwa wao katika siku zilizopita.