Rushwa yachangia mgogoro wa kidemokrasia duniani
29 Januari 2019Shirika la kimataifa la Transparency International limetoa ripoti mpya inayoangazia rushwa katika viwango vya kimataifa. Ripoti hiyo imebainisha hali ya kutisha kuhusu vitendo vya rushwa duniani kwa kusema theluthi moja ya nchi 180 zilipata alama chini ya 50 kati ya 100 wakati alama za wastani kwenye nchi zote zikiwa ni ndogo sana 43.
Kwenye faharasa yake kuhusu ufisadi ambayo imechapishwa leo, Transparency International ambayo ni taasisi isiyo ya kiserikali imesema kushindwa kwa jumla katika kudhibiti rushwa kunachangia mgogoro wa kidemokrasia duniani kote.
Kwa kuzingatia maeneo ya kikanda nchi za Ulaya ya Magharibi na hasa za Umoja wa Ulaya, ndizo zimepata wastani wa alama 66. Na zilizoshika mkia ni nchi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, zikiwa na wastani wa alama 33.
Ahadi za Afrika dhidi ya ufisadi hazijatekelezeka
Kwa mujibu wa ripoti hiyo bara la Afrika limeshindwa kutafsiri ahadi zake za kupambana na rushwa katika maendeleo halisi.
Mwanaharakati wa kupambana na ufisadi nchini Kenya Okiya Omutata amesema vita dhidi ya rushwa vinaendeshwa kwa maneno tu bila matendo kando na kuwa haviendeshwi kwa uwazi na ukweli. ''Siasa nyingi ndizo zinapigwa. Hatuoni kazi ikifanyika kama inavyostahili. Ukiangalia mashtaka kortini, pia hayana uzito, ushahidi haupo, na ukiangalia wanajaribu tu kuonyesha kuwa wanafanya kai, lakini si kwamba wanataka kuungoa ufisadi na mzizi wake ili utupwe mbali''
Nchi zilizoonekana kuwa na viwango vya juu vya rushwa ni zile zinazokabiliwa na vita za Somalia, Sudan Kusini na Syria.
Ripoti hiyo pia imetaja kwamba, mara nyingi, taasisi nyingi za kidemokrasia hutishiwa ulimwenguni kote na viongozi wenye tabia za kutumia nguvu au wenye misimamo mikali.
Mkurugenzi wa Transparency International, Patricia Moreira amesema juhudi zaidi zinahitajika ili kuimarisha ukaguzi na uwajibikaji kwa ajili ya kulinda haki za raia.
Denmark na New Zealand zaongoza katika vita dhidi ya ufisadi
Denmark na New Zealand zimeendelea kuongoza kuwa nchi zenye vitendo vichache vya rushwa katika miaka ya hivi karibuni na ziliongoza pia mwaka uliopita wa 2018, Denmark ikiwa na pointi pointi 88, na New Zealand ya pili kwa kuwa na pointi 87. Finland, Singapore, Sweden, Uswisi, Norway, Uholanzi, Kanada, Luxembourg, Ujerumani na Uingereza zinashikilia nafasi 10 za juu.
Ni mara ya kwanza kwa Marekani kutoingia kwenye nchi 20 zisizokuwa na hali mbaya ya ufisadi tangu mwaka 2011.
Nchi za Asia ya Pacific zina alama 44 wakati Ulaya ya Mashariki, Asia ya kati zikiwa na wastani wa alama 35. Nchi za Amerika pia zina wastani wa alama 44.
China imepata wastani wa alama 39 na hivyo kushika nafasi ya 87 nyuma ya india iliyo katika nafasi ya 78 kwa kupata wastani wa alama 41. Urusi iko kwenye nafasi ya 138.
Ripoti imezitolea mwito serikali kuyapa kipaumbele maeneo manne katika kupambana na rushwa:
• Kuimarisha taasisi zinazofuatilia nguvu za kisiasa.
• Kuziba pengo la utekelezaji kati ya sheria ya kupambana na rushwa, na utekelezaji wake.
• Kuyasaidia mashirika ya kiraia ambayo yanahamasisha ushirikiano wa kisiasa na ufuatiliaji wa umma juu ya matumizi ya serikali.
• Kuunga mkono uhuru wa vyombo vya habari
Mwandishi: John Juma/DW
Mhariri: Iddi Ssessanga