Rumsfeld: Wamarekani hawatoihama Iraq Juni 30
14 Februari 2004Matangazo
WASHINGTON: Waziri wa Mambo ya Ulinzi wa Marekani Donald Rumsfeld amefafanua kwamba hata kama Marekani ina niya ya kuikabidhi Iraq madaraka yake hapo Juni 30, lakini haina maana kuwa itahamisha wanajeshi wa Kimataifa wanaoongozwa na Marekani. Bwana Rumsfeld aliliambia Baraza la Bunge la Marekani kuwa bado haikuwekwa tarehe ya kuhamishwa wanajeshi. Hapo jana, yule mjumbe maalumu wa UM kwa Iraq, Lakhdar Brahimi alionya kuhusu kitisho cha kuweza kutokea vita vya ndani nchini Iraq kwa sababu ya kuzidi uhasama kati ya makabila mbali mbali. Baada ya kufanya mazungumzo pamoja na kiongozi wa kidini wa madhehebu ya Washiya, Ayatollah Ali Sistani, Bwana Brahimi alidokeza kuwa haungi mkono kuwa uchaguzi ufanyike kabla ya Juni 30. Ripoti rasmi inatazamiwa baada ya siku 10. - Watu 15 waliuawa na zaidi ya 20 kujeruhiwa hii leo yaliposhambuliwa kituo cha polisi na jengo la kiserikali mjini Falluja, kwa mujibu wa ripoti za mahospitali.