Rubio: Matumaini ya mwafaka Ukraine ni madogo mno
16 Mei 2025Katika ujumbe wa video alioutoa kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram, Medinsky amesema wako tayari kufanya kazi na kwamba hapo Alhamis walikuwa na mazungumzo mazuri na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan.
Urusi haiko tayari kuvimaliza vita
Kwa upande wake Ukraine kupitia Rais Volodymyr Zelenskiy imesema, inautuma ujumbe wake unaoongozwa na waziri wa ulinzi Rustem Umerov, licha ya kuwa ujumbe wa Moscow haujumuishi yeyote anayefanya maamuzi kuhusiana na vita vya Ukraine.
Zelenskiy amesema lengo la ujumbe wake ni kujaribu kufanikisha hatua za awali za usitishwaji mapigano.
Zelenskiy ambaye hapo Alhamis alisafiri kwenda Uturuki baada ya kumtaka Rais wa Urusi Vladimir Putin wafanye mazungumzo ya ana kwa ana huko Ankara, ameituhumu Moscow kwa kutofanya juhudi za kweli za kufikisha mwisho vita hivyo, kwa kutuma ujumbe wa ngazi ya chini kwa mazungumzo hayo ya amani, aliyoyaitisha Putin mwenyewe.
Haya yanafanyika wakati ambapo waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio amesema matumaini ni madogo mno kwa mazungumzo hayo ya amani kutoa mwafaka, baada ya pande hizo mbili kushambuliana kwa maneno kuelekea mazungumzo hayo.
Kuelekea kufanyika mazungumzo hayo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharova amemuita Zelenskiy "kikaragosi" huku waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov akimtaja rais huyo wa Ukraine kama mtu "mbaya" kwa kumshurutisha Putin kuhudhuria mazungumzo hayo binafsi.
Ila Zelenskiy amesisitiza kuwa, Putin ni sharti aonyeshe uongozi wake na ahudhurie mkutano huo iwapo kweli yuko tayari kwa mazungumzo.
Mazungumzo ya kwanza tangu 2022
Haijabainika ni mazungumzo ya aina gani yatakayofanyika kwa sasa ukizingatia Putin na Zelenskiy wote hawatokuwepo, ila maafisa wa Uturuki wamesema upo uwezekano wa mazungumzo ya mataifa matatu Ukraine, Urusi na Uturuki kufanyika Ijumaa.
Rais wa Marekani Donald Trump kama waziri wake wa mambo ya kigeni Rubio, ameonekana kutilia shaka upatikanaji wa suluhu katika vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya miaka mitatu sasa, akikiri kuwa huenda mwafaka usipatikane hadi pale atakapokutana na Rais Putin.
Makumi kwa maelfu ya watu wameuwawa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari mwaka 2022 na Urusi kwa sasa inakalia angalau asilimia 20 ya ardhi ya Ukraine.
Hakujawa na mazungumzo ya ana kwa ana ya amani kati ya pande hizo mbili tangu mkutano uliofanyika katika wiki za mwanzo za vita hivyo na kutokea wakati huo, nchi hizo mbili zimeonekana kuzidi kutofautiana kimsimamo.
Zelenskiy atahudhuria mkutano wa viongozi wa Ulaya katika Mji Mkuu wa Albania, Tirana, siku ya Ijumaa.
Vyanzo: AFP/AP/Reuters