Rubio kuijadili Ukraine na viongozi wa Ufaransa
17 Aprili 2025Rubio pamoja na mjumbe maalumu wa Rais Donald Trump, Steve Witkoff pia watajadili wasiwasi kuhusu mradi wa nyuklia wa Urusi na mzozo wa Mashariki ya Kati watakapokutana na Rais Emmanuel Macron na waziri wake wa mambo ya nje Jean-Noel Barrot.
Taarifa hizo zimetolewa na chanzo kimoja cha kidiplomasia kilichozungumza na shirika la habari la AFP. Mazungumzo hayo yatafanyika chini ya kiwingu cha kusuasua kwa jitahada za kuishawishi Urusi ikubali usitishwaji mapigano kwa muda. Yanafanyika siku kadhaa tangu Urusi ilipoishambulia miji miwili ya Ukraine na kusababisha vifo vya makumi ya watu.
Mataifa ya Ulaya ikiwemo Ufaransa yalikosoa kwa matamshi makali mashambulizi hayo na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa alisema jana Jumatano kwamba Rais Vladmiri Putin ameonesha kwa mara nyingine "kuwa ukatili wake hauna mipaka na hana dhamira ya kusitisha vita."