Rubio afanya mazungumzo na Lavrov kuhusu vita vya Ukraine
10 Julai 2025Mwanadiplomasia huyo wa Marekani ameyasema hayo wakati alipokutana na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov.
Rubio ameeleza kuwa mazungumzo yaliyodumu dakika 50 kati yake na Lavrov yaliyofanyika kando ya mkutano wa mawaziri wa nje wa Jumuiya ya mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia ASEAN nchini Malaysia yalikuwa "wazi na muhimu.”
Alimuelezea Lavrov kile Rais Donald Trump alichosema wazi kwamba, Urusi haijaonyesha utayari wa kuvimaliza vita hivyo.
Mkutano huo wa pili wa ana kwa ana kati ya wanadiplomasia hao umefanyika katikati ya ongezeko la mashambulizi ya Urusi nchini Ukraine. Trump ameonyesha kukerwa na Rais Vladimir Putin kwa kuviendelea vita hivyo.
Mwanadiplomasia huyo wa Marekani ameongeza kuwa, wamebadilishana mawazo na Lavrov ikiwemo kile alichokiita "njia mpya au tofauti” kutoka upande wa Urusi ya kuvimaliza vita, ambayo ataiwasilisha kwa Trump pindi atakaporudi Washington.
"Tunahitaji kuona ramani ya kuelekea kuumaliza mzozo huu,” aliongeza kusema Rubio.
Urusi yaishambulia Ukraine kwa makombora
Mapema Alhamisi, Urusi iliushambulia mji mkuu wa Ukraine, Kyiv kwa makombora na droni, hali iliyolazimisha maelfu ya watu nchini Ukraine kutafuta hifadhi katika makaazi ya dharura.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy aliweka wazi kwamba Urusi ilirusha makombora 18 na droni 400 wakati wa shambulio hilo lililolenga mji mkuu wa Kyiv.
Hata hivyo hakukuwepo na tamko lolote kutoka Moscow kufuatia shambulio hilo, siku moja tu baada ya Urusi kufanya shambulio lengine kwa kutumia droni 728 - idadi kubwa zaidi ya droni kuwahi kutumika, dhidi ya jirani yake huyo.
Trump aliyerejea madarakani mwaka huu, kwa ahadi ya kuvimaliza vita kati ya Urusi na Ukraine haraka iwezekanavyo, ameonekana kutokuwa na msimamo mkali dhidi ya Urusi ikilinganishwa na mtangulizi wake Joe Biden, ambaye alikuwa akiiunga mkono kwa dhati Ukraine.
Hivi karibuni baada ya Trump kuidhinisha kuendelea kwa misaada ya silaha kwa Ukraine, kiongozi huyo wa Marekani aliikosoa vikali Moscow, akisema matamshi ya Putin kuhusu amani, "hayana maana.”