Mashambulizi ya RSF yalaaniwa vikali
14 Aprili 2025Idadi hiyo ya vifo ni kulingana na Mtandao wa Wanaharakati wa masuala ya wanawake kwenye Pembe ya Afrika la Strategic Initiative for Women, SIHA.
SIHA liliarifu siku ya Jumamosi kwamba, kwenye shambulizi hilo la siku ya Ijumaa, RSF walichoma moto jiko linalotumiwa na jamii ya wakimbizi walioko kwenye kambi hiyo iliyoko kwenye jimbo la Darfur Kaskazini na kuwauwa wafanyakazi wa kujitolea, miongoni mwao alikuwa ni mama mjamzito.
Muungano wa mashirika zaidi ya 70 ya misaada nchini Sudan, INGO Forum umesema zaidi ya watot 20 waliuawa kwenye shambulizi hilo la kambi ya Zamzam. Taarifa yake ilisema raia wanakabiliwa na njaa kali, wanauliwa na kuzuiwa kuondoka. Lakini pia wafanyakazi wa kujitolea nao wanawindwa usiku na mchana na kusema hayo yote hayakubaliki hata kidogo kwa kuwa yanakiuka sheria za kimataifa.
Karibu wakimbizi 500,000 wanaishi kwenye kambi ya Zamzam
Karibu wakimbizi 500,000 wanaishi kwenye kambi hiyo, ingawa baadhi wakadiria kwamba huenda idadi yao ikafikia milioni moja.
Mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, Al Fasher umezingirwa na RSF kwa karibu mwaka mmoja sasa, katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan.
Afisa wa jumba la makumbusho la Kitaifa Gamal ElDeen Zain al-Abdeen anasema, pamoja na uhalifu wa kibinaadamu, hata eneo anallolisimamia nalo limeharibiwa kwa mashambulizi ya RSF.
"Wanamgambo hawa wa RSF wameharibu kila kitu ikiwa ni pamoja na kila kitu kinachomuhusu mtu binafsi wa Sudan na ustaarabu wa watu wa Sudan."
Jana Jumapili, RSF ilitangaza kuidhibiti kambi ya Zamzam baada ya siku mbili za mapigano makali. Kwenye taarifa yao, RSF walisema ilipeleka wanajeshi kwa ajili ya kuwanusuru raia na wafanyakazi wa afya na misaada ya kiutu baada ya kuikomboa kambi hiyo kutoka kwenye mikono ya jeshi.
RSF imezidisha mashambulizi katika kambi za wakimbizi
RSF ilianzisha mashambulizi Ijumaa iliyopita katika mji wa El-Fasher, Zamzam iliyoko karibu na mji huo, pamoja na kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abu Shouk. Kulingana na Umoja wa Mataifa, karibu watu 100 wanahofiwa kuuawa.
RSF wameongeza mashambulizi katika wiki za karibuni kwenye makambi ya wakimbizi katika mji wa Al-Fasher, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kukamata mji huo mkuu na ambao ni wa mwisho huko Darfur, ambao hauko chini ya mamlaka yake.
Wakimbizi wa eneo hilo wamelielezea shambulizi hili la karibuni kuwa baya kabisa lililowafanya kuanza safari ya siku tatu ya karibu kilomita 80 ili kuyanusuru maisha yao.
Mapigano makali ya kuwania madaraka yamelikumba taifa hilo kwa miaka miwili sasa kati ya mtawala na mkuu wa jeshi, Jenerali Abdel Fattah al-Burhan dhidi ya swahiba na makamu wake wa zamani Hamdan Daglo anayeongoza wanamgambo wa RSF.
Kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, mzozo huo umesababisha zaidi ya watu milioni 12.5 kuyakimbia makazi yao, huku mapigano yakizidi kusambaa, tena kwa viwango tofauti.
Umoja wa Mataifa unasema ni mapigano yaliyobua mzozo mkubwa kabisa wa kibinaadamu, katika wakati ambao kati ya wakazi milioni 51 wa Sudan, asilimia 64 inategemea misaada ya kiutu, huku wanawake na wasichana wakiwa ni waathirika wakubwa na hasa wa unyanyasaji wa kingono unaofanywa na makundi ya wabakaji.
Bado idadi dhahiri ya vifo haijulikani, lakini mashirika ya misaada ya kimataifa yanasema ni kati ya 40,000 hadi 150,000.