RSF: Jeshi la Uganda liliwashambulia waandishi
21 Machi 2025Taarifa ya shirika hilo limesema waandishi hao "walipigwa vibaya" na wanajeshi na maafisa wa idara ya kupambana na ugaidi wa Uganda walipokuwa kazini kufuatilia uchaguzi wa jimbo la Kawempe Kaskazini uliofanyika Machi 13.
Mpiga picha wa gazeti la kila siku la nchini Uganda, Daily Monitor, Abubaker Lubowa ameliambia shirika la RSF kuwa askari waliwalazimisha kuvua mashati na wayatumie kufunika macho, wakawaamuru kulala chini na kuwashambuliwa kwa bakora na vitako vya bunduki.
Soma pia: Uhuru wa vyombo vya habari wazidi kudidimia duniani
Simulizi sawa na hiyo imetolewa pia na mwandishi mwingine wa kituo cha televisheni cha Uganda NTV alipozungumza na RSF.
Mkuu wa shirika hilo kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara, Sadibou Marong ametaka uchunguzi kufanyika akisema ukatili uliofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya waandishi hao wa habari ni kitendo kisichokubalika.