Risasi za Israel zawaua watu 93 katika Ukanda wa Gaza
21 Julai 2025Matangazo
Wakala wa ulinzi wa Gaza umesema vikosi vya Israel vimefyetua risasi dhidi ya umati wa Wapalestina waliokuwa wakijaribu kuchukua chakula cha msaada katika eneo hilo lililokabiliwa vita na kuwauwa watu 93 na kuwajeruhi wengine kadhaa jana Jumapili.
Shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, limesema msafara wa malori 25 yaliyokuwa yamebeba chakula yalikutana na makundi ya raia wanaokabiliwa na njaa ambao walishambuliwa kwa risasi karibu na mji wa Gaza, muda mfupi baada ya kuvuka kutokea Israel na kupita vituo vya upekuzi.
Jeshi la Israel limetilia shaka takwimu za vifo likisema wanajeshi wake walifyetua risasi kama onyo kuondosha kitisho cha haraka kilichowakabili wakati maalfu ya watu walipokusanyika karibu na mji wa Gaza.