Haki za wanawake hatarini miaka 30 tangu azimio la Beijing
6 Machi 2025Miaka 30 tangu viongozi wa dunia walipopitisha mpango wa kihistoria wa kufanikisha usawa wa kijinsia, ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa inaonyesha kuwa haki za wanawake na wasichana ziko katika hatari kubwa.
Ripoti hiyo, iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa linalojihusisha na masuala ya Wanawake, UN Women, inabainisha kuwa takribani robo ya serikali duniani zimeripoti kushuhudia kurudi nyuma kwa haki za wanawake mwaka uliopita, huku ubaguzi wa kijinsia ukiendelea kuenea katika jamii na mifumo ya kiuchumi.
Licha ya maendeleo fulani, kama vile upatikanaji wa elimu kwa wasichana na huduma za uzazi wa mpango, bado changamoto ni kubwa. Ripoti inaonyesha kuwa kila baada ya dakika 10, mwanamke au msichana huuawa na mwenza wake au mwanafamilia.
Aidha, matukio ya ukatili wa kingono yanayohusiana na migogoro yameongezeka kwa asilimia 50 tangu mwaka 2022. Zaidi ya hayo, ni nchi 87 pekee ambazo zimewahi kuongozwa na mwanamke, jambo linaloashiria pengo kubwa katika uongozi wa kisiasa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisisitiza kuwa badala ya kuimarisha usawa wa haki za binadamu, dunia inashuhudia kuenea kwa chuki dhidi ya wanawake. Aliitaka jumuiya ya kimataifa kusimama kidete kuhakikisha haki za wanawake na wasichana zinaheshimiwa kwa wote, kila mahali.
Mwaka 1995, nchi 189 zilihudhuria mkutano wa wanawake wa Beijing na kupitisha azimio la kurasimisha haki za wanawake, likiwataka viongozi kuchukua hatua madhubuti katika maeneo 12, ikiwa ni pamoja na kutokomeza umaskini, kupinga ukatili wa kijinsia, na kuwaweka wanawake katika nafasi za maamuzi. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Umoja wa Mataifa, hati hiyo ilitambua kwamba haki za binadamu zinajumuisha uwezo wa wanawake kuamua kuhusu afya yao ya uzazi na masuala yanayohusiana na maisha yao ya kijinsia bila ubaguzi au shinikizo.
Changamoto zinazoendelea kuhujumu usawa wa kijinsia
Katika mapitio mapya, ripoti hiyo inabainisha kuwa nchi nyingi zimepiga hatua katika usawa wa kijinsia katika miaka mitano iliyopita, huku asilimia 88 ya mataifa yakiwa yamepitisha sheria za kupambana na ukatili wa kijinsia na kuanzisha huduma za kusaidia waathirika. Pia, asilimia 44 ya nchi zimeimarisha elimu na mafunzo kwa wasichana na wanawake. Hata hivyo, ripoti inasisitiza kuwa usawa wa kijinsia bado unakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa rasilimali na nafasi za maamuzi kwa wanawake.
Ripoti inaeleza kuwa kuzorota kwa demokrasia kumeenda sambamba na kurudi nyuma kwa haki za wanawake. Wanaharakati wa kupinga haki za wanawake wanapinga sera na sheria zinazoendeleza usawa wa kijinsia. Asilimia 25 ya mataifa yameripoti kuwa upinzani huu unakwamisha utekelezaji wa Azimio la Beijing. Ingawa idadi ya wabunge wa kike imeongezeka mara mbili tangu 1995, bado theluthi tatu ya wabunge duniani ni wanaume.
Soma pia: UN: Idadi ya wanawake na wasichana wanaoathirika na vita yaongezeka
UN Women inasema kuwa wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanaendelea kukosa fursa za uzazi wa mpango wa kisasa, huku kiwango cha vifo vya wajawazito kikiwa hakijabadilika tangu mwaka 2015. Asilimia 10 ya wanawake na wasichana wanaishi katika umaskini uliokithiri. Ripoti pia inasema kuwa matukio ya ukatili wa kingono yanayohusiana na migogoro yameongezeka kwa asilimia 50 tangu 2022, ambapo asilimia 95 ya waathirika ni wanawake na wasichana.
Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women, Sima Bahous, anasema kuwa shirika lake limeandaa mpango wa utekelezaji ili kufanikisha lengo la Umoja wa Mataifa la usawa wa kijinsia ifikapo 2030. Mpango huo unahimiza mapinduzi ya kidijitali ili wanawake na wasichana wapate fursa sawa za teknolojia, uwekezaji katika ulinzi wa kijamii kama vile elimu bora na huduma za afya, kutokomeza ukatili wa kijinsia, ushiriki sawa katika maamuzi, na ufadhili wa misaada ya kibinadamu inayozingatia usawa wa kijinsia katika maeneo ya migogoro.