Ripoti: Kampuni ya Rwanda yauza madini ya Kongo
16 Aprili 2025Kulingana na taarifa zilizokusanywa na shirika hilo la Global Witness, kampuni ya Traxys ilinunua mwaka jana tani zipatazo 280 za coltan kutoka Rwanda, madini ambayo hutumiwa katika utengenezaji wa simu za mkononi na betri za magari ya umeme.
Hayo ni kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa kwenye takwimu za forodha pamoja na ushuhuda uliotolewa na wasafirishaji haramu wa madini ambao umebaini kuwa sehemu kubwa ya madini hayo ya coltan yalichimbwa katika maeneo yenye migogoro mashariki mwa Kongo, ambapo kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda linaendesha shughuli zake.
Kundi hilo la waasi ambalo linadhibiti maeneo kunakochimbwa madini mbalimbali huko Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC, linaonekana kufaidika kutokana na unyonyaji wa rasilimali hizo ili kufadhili operesheni zake za kijeshi.
Soma pia: Waasi wa M23 wanavyojinufaisha na madini ya Kongo
DW ilizumgumza na Alex Kopp, mtafiti katika shirika hilo la Global Witness aliefafanua ni namna gani biashara hiyo hufanyika.
"Tuliweza kuzungumza na mmoja wa wafanyabiashara ambaye alituthibitishia kuwa kampuni ya African Panther ya Rwanda hununua madini ya coltan huko Rubaya na kisha kuyauza kwa kampuni ya Traxys. Madini hayo ni kutoka migodi ya Rubaya ambayo inakaliwa na waasi wa M23 tangu Aprili mwaka jana."
Kopp ameongeza kuwa migodi ya Rubaya ni miongoni mwa migodi mikubwa zaidi ya coltan duniani ambapo Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa karibu asilimia 15 ya coltan inayozalishwa kote ulimwenguni hutoka kwenye migodi hiyo.
Kukanusha kwa Traxys na ripoti za Umoja wa Mataifa
Kampuni ya Traxys imekanusha uhusiano wowote na hata ufadhili kwa kundi la M23 na kukana madai kwamba madini hayo ya coltan yanatoka maeneo yenye migogoro nchini Kongo.
Lakini kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa lilichapisha ripoti inayothibitisha ukaliaji wa M23 katika migodi hiyo ya Rubaya na kwamba wachimbaji na wafanyabiashara hutakiwa kulipa ushuru kwa M23.
Soma pia: Nangaa: Vikwazo na mkataba wa madini havitamaliza vita Kongo
Ripoti hiyo inaendelea kuwa M23 husafirisha hadi nchini Rwanda takriban tani 120 za coltan kwa mwezi na ushuru unaotoza kwa uzalishaji huo huipatia mapato yanayokadiriwa kufikia dola za Kimarekani 800,000 kwa mwezi na hivyo kuifanya migodi hiyo kuwa sehemu kubwa ya mapato kwa kundi hilo la waasi wa M23.
Shirika la Global Witness limeibua pia wasiwasi kuhusu mahusiano kati ya Umoja wa Ulaya na Rwanda baada ya kutia saini mnamo Februari mwaka 2024, mpango wa ushirikiano wa kimkakati uliokuwa na lengo la kuwezesha upatikanaji wa malighafi.
Uchunguzi huu umebaini kwamba madini yaliyopatikana kwenye maeneo yenye mizozo, ikiwa ni pamoja na coltan, yameingia kwenye minyororo ya ugavi ya Umoja huo bila ya kuwepo hatua za kutosha za kuzuia jambo hilo.