Wanawake walidhulumiwa wakati na baada ya vita vya Tigray
3 Agosti 2025Mashirika mawili yasiyo ya kiserikali ya kutetea haki za binadamu yameelezea katika ripoti yao inayojumuisha "uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu."
Ripoti hiyo imesema eneo la kaskazini mwa Ethiopia lilikabiliwa na vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwaka 2020 hadi 2022, ambapo vikosi vya serikali ya Ethiopia, vilivyoungwa mkono na jeshi la Eritrea na wanamgambo wa ndani, vilihusika dhidi ya chama cha siasa cha eneo hilo, cha Tigray People's Liberation Front (TPLF).
Watu wapatao 600,000 walikufa wakati wa vita hivyo, na pande zote zililaumiwa kwa kufanya ukatili.
Ripoti hiyo ya kurasa 88 iliyoandaliwa na kundi la Madaktari wa Haki za Kibinadamu (PHR) na Shirika la Haki na Uwajibikaji katika Pembe ya Afrika (OJAH) inajumuisha mahojiano na wafanyakazi wapatao 500 wa huduma za afya na maafisa wa mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesaidia kufichua matendo ya unyanyasaji yaliyofanywa kwa makusudi ambayo yanaohusiana na unyanyasaji wa kijinsia na kuwapa wanawake mimba zisizotakiwa.
Mashirika ya kutetea haki ya PHR na OJAH yamesema kwenye ripoti yao kwamba:
"Vitendo hivyo vinajumuisha uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu kutokana na unyanyasaji wa kijinsia, mimba za kulazimishwa, utumwa wa kingono na mateso kwa kuzingatia misingi ya kikabila, jinsia, umri na misimamo ya kisiasa."
Lindsey Green, naibu mkurugenzi wa utafiti wa PHR, ameliambia shirika la habari la AFP, kwamba, "wahalifu wamefanya uharibifu bila kuadhibiwa na waathiriwa wamenyamazishwa."
Green ameyataka mashirika hayo kufanya uchunguzi zaidi ili kubaini kama uhalifu wa "mauaji ya kimbari" ulitekelezwa.
Amesema mashirika ya kutetea haki ya PHR na OJAH hayana data zitakazowezesha kufanya uamuzi huo, ingawa vipo viashiria vya wazi kwamba nia ya wahalifu ilikuwa ni kuwaangamiza jamii ya watu wa kabila la Tigrinya kutokana na majeraha ya kimwili yanayoonekana waliyopata watu wa jamii hiyo.
Je vurugu hizo zilifanywa na nani?
Ripoti hiyo imeeleza kwamba vurugu hizo mara nyingi zilifanywa na watu ambao wanazungumza lugha ya Kieritrea na walivaa sare zinazoonyesha uhusiano na jeshi la Eritrea.
Wahusika wengine ni pamoja na wanajeshi wa Ethiopia, pamoja na makundi mengine yanayoiunga mkono serikali, yakiwemo makundi yenye silaha kutoka eneo jirani la Amhara.
Waziri wa Habari wa Eritrea Yemane Ghebremeskel alikataa kuizungumzia ripoti hiyo alipoulizwa na AFP. Na msemaji wa jeshi la shirikisho la Ethiopia na msemaji wa mamlaka ya Amhara hawakujibu maswali waliyoulizwa.
Mratibu wa afya ya uzazi huko Tigray aliwaambia watafiti wa ripoti hiyo kwamba "wahalifu hawakuchochewa na tamaa ya ngono bali na hamu ya kuleta maumivu na mateso kwa wanawake walionyanyaswa kijinsia."
Mwanasaikolojia wa jimbo la Tigray amesema wapo wanawake waliobakwa na askari huku kaka zao au waume zao wakilazimishwa kushuhudia maonevu hayo.
Ripoti ya mashirika ya Madaktari wa Haki za Kibinadamu (PHR) na Shirika la Haki na Uwajibikaji katika Pembe ya Afrika (OJAH) imesema ukatili unaendelea katika mikoa kadhaa ya nchini Ethiopia kutokana na ukosefu wa uwajibikaji.
Chanzo: AFP