Ripoti: Marekani yapanga kuchukua udhibiti kamili wa Gaza
1 Septemba 2025Marekani inapanga kuwahamisha wakaazi wote wa ukanda wa Gaza na kuchukua udhibiti kamili wa ukanda huo chini ya mpango unaozingatiwa na utawala wa Rais Donald Trump.
Taarifa hizo zimeripotiwa jana Jumapili na gazeti la The Washington Post.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, mpango huo umebuniwa kufuatia kauli ya Trump ya kuifanya Gaza kuwa "Riviera ya Mashariki ya Kati.” Lengo kuu ni kuibadilisha Gaza – ardhi ambayo Wapalestina wanataka iwe sehemu ya taifa lao la baadaye – kuwa kituo cha utalii na teknolojia ya kisasa.
Ukanda wa Gaza ambao umegeuzwa kuwa kifusi kufuatia mashambulizi ya Israel yaliyochochewa na shambulio la Hamas la mwaka 2023, unatarajiwa kuwa chini ya usimamizi wa Marekani kwa angalau miaka 10, gazeti hilo limeripoti.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameusifu mpango huo wa Marekani, ambao hata hivyo umekosolewa vikali na mataifa mengi ya Ulaya na Kiarabu, yakieleza wasiwasi kuhusu athari zake kwa wakaazi wa Gaza na mustakabali wa eneo hilo.