Ripoti:Nchi nyingi kuathrika baada ya Marekani kufuta msaada
12 Februari 2025Kituo cha Maendeleo ya Kimataifa chenye makao yake makuu jijini Washington CGD, kimeonya kwamba kusitishwa kwa misaada ya kigeni ya Marekani na uwezekano wa kuvunjwa kwa shirika la misaada ya kimataifa la USAID, kutayaathiri pakubwa baadhi ya mataifa maskini duniani.
Soma: Athari za ukataji misaada wa Marekani kwa Uganda
Kituo hicho kimesema katika taarifa yake kwamba kusitisha kwa mwaka mzima kwa msaada wa Marekani kunaweza kumaanisha hasara ya zaidi ya asilimia moja ya pato la taifa kwa nchi zipatazo 20 duniani.
Chini ya wiki moja baada ya Rais Donald Trump kurejea Ikulu ya Marekani, USAID imeyaeleza mashirika yasiyo ya kiserikali kwamba watalazimika kusitisha shughuli zake mara moja baada ya utawala mpya kusimamisha bajeti zake.
Hayo yanajiri wakati mkaguzi mkuu wa shirika la USAID Paul Martin akiondolewa kutoka katika nafasi yake.