Ripoti: Idadi kubwa ya watu duniani huvuta hewa chafu
11 Machi 2025Ripoti hiyo iliyotolewa Jumanne (11.03.2025) na shirika la IQAir Global lenye makao yake nchini Uswisi ambalo hufuatia na kukusanya data za uchafuzi wa hewa, inaeleza kuwa sehemu kubwa ya dunia ina hewa chafu huku asilimia 17 tu ya miji duniani kote ndiyo huheshimu miongozo kuhusu uchafuzi wa hewa.
Shirika hilo la IQAir Global lilikusanya data kutoka vituo 40,000 vya ufuatiliaji wa ubora wa hewa katika nchi 138 na kugundua kuwa mataifa ya Chad, Kongo, Bangladesh, Pakistan na India yalikuwa na hewa chafu zaidi. Miji sita kati ya tisa ya India ilichafuliwa zaidi huku mji wa viwanda wa Byrnihat kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ukiwa katika hali mbaya zaidi.
Wataalam wanasema huenda hali halisi ya uchafuzi wa hewa ni kubwa zaidi kuliko inavyoelezwa hasa ikizingatiwa kuwa sehemu nyingi za dunia hazina vifaa vya ufuatiliaji vinavyotoa data kwa usahihi zaidi, mfano barani Afrika kuna wastani wa kituo kimoja tu cha ufuatiliaji kwa idadi ya watu milioni 3.7.
Ripoti hiyo hata hivyo imesema kuwa vifaa zaidi vya kukusanya data kuhusu ubora wa hewa vinaendelea kuwekwa sehemu mbalimbali duniani ili kukabiliana na tatizo hilo. Mwaka huu, ripoti hiyo iliweza kujumuisha data kutoka maeneo mapya 8,954 ikiwa ni matokeo ya juhudi za kufuatilia vyema uchafuzi wa hewa. Lakini wiki iliyopita, ufuatiliaji wa data hizo ulipata pigo wakati Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilipotangaza kuwa haitotangaza mkusanyiko wa data kutoka vifaa mbalimbali vilivyopo kwenye balozi zake kote ulimwenguni.
Wanasayansi: "Kuvuta hewa chafu kwa muda mrefu kunasababisha magonjwa"
Fatimah Ahamad, mwanasayansi mkuu na mtaalam wa uchafuzi wa hewa katika Kituo cha Sunway nchini Malaysia anasema kupumua hewa chafu kwa muda mrefu kunaweza kusababisha magonjwa yanayoathiri mfumo wa kupumua, ugonjwa wa Alzheimer na hata saratani. Shirika la Afya Duniani WHO linakadiria kuwa uchafuzi wa hewa husababisha vifo vya karibu watu milioni 7 kila mwaka.
Soma pia: Mataifa ya dunia yakosa mwafaka kuhusu mazingira
Awali, WHO iligundua kuwa asilimia 99% ya idadi ya watu duniani wanaishi katika maeneo ambayo hayafikii viwango vya ubora wa hewa vilivyopendekezwa na shirika hilo. Miji kama Beijing, Seoul na Rybnik huko Poland imefanikiwa hata hivyo kuboresha hewa kwa kuchukua hatua na kuweka kanuni kali kuhusu uchafuzi wa mazingira utokao kwenye magari, mitambo ya kuzalisha umeme na hata viwanda.
Pia miji hiyo imewekeza katika miradi ya nishati safi pamoja na jitihada nyingine mashuhuri za kuzuia uchafuzi mkubwa wa hewa. Makubaliano ya Muungano wa Mataifa ya Kusini-Mashariki mwa Asia juu ya uchafuzi wa kuvuka mipaka ulisaidia pia. Ingawa kwa sasa mafanikio yake bado ni madogo, nchi kumi katika kanda hiyo ziliahidi kufanya kazi pamoja ili kufuatilia na kudhibiti uchafuzi wa mazingira kutokana na mioto mikubwa ya nyika ambayo hushuhudiwa eneo hilo wakati wa kiangazi.
Soma pia: Uchafuzi wa hewa huchochea saratani ya mapafu kati ya wasiovuta sigara
Akiielezea ripoti ya mwaka huu, Frank Hammes, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la IQAir Global amesema:
"Matokeo muhimu ya ripoti ya mwaka huu ni kwamba tumeona maendeleo chanya katika sehemu nyingi za dunia. Kwa bahati mbaya, maendeleo hayo yalikuwa madogo. Na tumeona kwamba sehemu nyingi za dunia ikiwa ni pamoja na Pakistan na India, kwa kweli hatujapiga hatua katika suala la ubora wa hewa. Huko Marekani, tumeona maendeleo makubwa kwa sababu hakukuwa na matokeo makubwa ya mioto ya nyika."
Mwanasayansi Ahamad anaendelea kusema kuwa bado kuna mambo mengi zaidi yanayohitajika kufanywa ili kupunguza viwango vya uchafuzi wa hewa, akikumbushia kuwa ikiwa hakuna maji safi, unaweza kuwaambia watu wasubiri nusu saa kwa siku na maji yatakuja. Lakini ikiwa una hewa chafu, huwezi kuwaambia watu wasitishe kupumua kwa muda.
Kwa upande wake Shweta Narayan, Mratibu wa kampeni katika shirika la Global Climate and Health Alliance, anasema maeneo mengi yanayoshuhudia uchafuzi mbaya zaidi wa hewa huwa ni mahali ambapo gesi chafuzi hutolewa kwa wingi kupitia uchomaji wa makaa ya mawe, mafuta na gesi. Anasisitiza kuwa ili kupunguza joto kali inayoiathiri dunia tunapaswa kupunguza pia uzalishaji wa hewa chafu ya kaboni ambayo amesema ni hatari kwa mazingira.
(Chanzo: AP)