Kongo na Rwanda zawasilisha rasimu ya amani kwa Marekani
6 Mei 2025Kongo na Rwanda zimewasilisha rasimu ya makubaliano ya amani kama sehemu ya mchakato unaoongozwa na Marekani, ambao huenda ukaumaliza mzozo unaoendelea mashariki mwa Kongo, eneo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali, afisa mmoja wa Marekani alisema Jumatatu.
Mshauri mwandamizi wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu masuala ya Afrika na Mashariki ya Kati, Massad Boulos, alisema kupitia mitandao ya kijamii kuwa amekaribisha rasimu hiyo "iliyopokelewa kutoka pande zote mbili – Kongo na Rwanda," akiitaja kuwa "hatua muhimu."
Maelezo ya rasimu hiyo hayakufahamika mara moja, ikiwa ni pamoja na iwapo inatoa nafuu kwa upatikanaji wa madini muhimu ya eneo hilo kwa ajili ya Marekani — jambo ambalo Rais wa Congo Félix Tshisekedi ameashiria kuwa linaweza kufanikishwa endapo Marekani itasaidia kutuliza hali ya vurugu.
Mgogoro wa muda mrefu mashariki mwa Kongo ulizidi kushika kasi mwezi Januari, wakati waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda walipouteka mji wa kimkakati wa Goma, na kufuatiwa na Bukavu mnamo Februari. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya takriban watu 3,000 na kuzua hofu ya kuzuka kwa vita vya kikanda.
Mashariki mwa Kongo imekumbwa na mizozo ya mara kwa mara kwa miongo kadhaa. Makundi kadhaa yenye silaha yanapigania maeneo yenye machimbo karibu na mpaka wa Rwanda. Mzozo huu umesababisha mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani, ambapo zaidi ya watu milioni 7 wamekosa makazi, ikiwa ni pamoja na 100,000 waliokimbia mwaka huu pekee.
Soma pia:Tshisekedi atetea mkataba wa amani kati ya Kongo na Rwanda
Kongo ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa uzalishaji wa madini ya cobalt, yanayotumika kutengeneza betri za magari ya umeme na simu za mkononi. Pia ina hifadhi kubwa ya dhahabu, almasi, na shaba.
Mazungumzo ya amani yachukua hatua mpya
Rasimu hiyo ya amani ya Jumatatu inakuja baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kusimamia utiaji saini wa ahadi kati ya Kongo na Rwanda mwezi uliopita, ya kushirikiana kuelekea makubaliano ya amani.
Waziri wa mambo ya nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, aliiambia Shirika la Utangazaji la Rwanda (RBA) Jumatatu kuwa atakutana na mwenzake wa Kongo wiki ya tatu ya Mei kujadili makubaliano ya mwisho ya amani.
Aliongeza kuwa anatumaini marais wa Rwanda na Kongo watasaini mkataba huo katikati ya mwezi Juni Ikulu ya White House mbele ya Rais Trump na viongozi wengine wa kikanda.
"Tuna matumaini kuwa mambo yakienda vyema, tutapata makubaliano ya amani yatakayowezesha amani ya kudumu katika eneo hili," alisema Nduhungirehe.
Hakukuwa na tamko lolote kutoka kwa mamlaka za Kongo kufikia wakati huo.
Waasi wa M23 wanaripotiwa kupata msaada kutoka kwa wanajeshi takriban 4,000 kutoka Rwanda, kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, na mara kadhaa wameapa kusonga hadi mji mkuu wa Kongo, Kinshasa, ulio umbali wa karibu kilomita 1,600 kuelekea magharibi.
Soma pia: Serikali ya Kongo na waasi wa M23 wakutana nchini Qatar
Kongo na Rwanda wanatumaini kuwa ushiriki wa Marekani — pamoja na motisha ya uwekezaji mkubwa endapo kutakuwa na usalama wa kutosha kwa kampuni za Kimarekani kufanya kazi mashariki mwa Congo — utapunguza machafuko ambayo yameshindikana kudhibitiwa na walinda amani wa kimataifa na juhudi za kidiplomasia tangu miaka ya 1990.
"Amani ya kudumu ... itafungua milango kwa uwekezaji mkubwa kutoka Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla, jambo litakalowezesha fursa za kiuchumi na ustawi," alisema Rubio, akiongeza kuwa hatua hiyo "itasongesha ajenda ya ustawi ya Rais Trump kwa dunia."
Baadhi ya wachambuzi wameonya kuwa Marekani inaweza kujikuta ikijihusisha au hata kuchochea zaidi vurugu za makundi ya waasi, ufisadi, unyonyaji na ukiukwaji wa haki za binadamu unaohusiana na uchimbaji wa madini mashariki mwa Kongo.
Wakati huohuo Jumatatu, mamlaka za Rwanda zimethibitisha kuwa mazungumzo yanaendelea na Marekani kuhusu makubaliano ya kuwapokea wahamiaji waliorejeshwa kutoka mataifa mengine.